×

Uswisi Yaiondoa Colombia kwa Penalti, Yatinga Robo Fainali kwa Mara ya Kwanza Tangu 1954


Uswisi imeandika historia kwa kutinga robo fainali ya Kombe la Dunia 2026 baada ya kuichapa Colombia kwa mabao 4-3 kwa mikwaju ya penalti kufuatia sare tasa ya 0-0 ndani ya dakika 120 za mchezo uliopigwa Vancouver.

Ni mara ya kwanza kwa Uswisi kufuzu hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia tangu ilipoandaa mashindano hayo mwaka 1954. Sasa itakutana na mabingwa watetezi Argentina katika robo fainali itakayopigwa Jumamosi mjini Kansas City.

Mchezo huo ulikuwa wa ushindani mkubwa huku pande zote zikishindwa kupata bao ndani ya muda wa kawaida na ule wa nyongeza.

Colombia ilianza kutengeneza nafasi mapema, lakini kipa Gregor Kobel aliokoa hatari kadhaa muhimu, ikiwemo shuti la Gustavo Puerta.
Katika kipindi cha pili na muda wa nyongeza, timu zote ziliendelea kushambuliana.

Jhon Lucumi wa Colombia alipiga mpira uliogonga mwamba wa lango, huku Jaminton Campaz akizuiwa na Kobel. Kwa upande wa Uswisi, Ruben Vargas na Zeki Amdouni walitengeneza nafasi lakini walishindwa kuzitumia.

Katika mikwaju ya penalti, Davinson Sanchez wa Colombia alipiga mpira uliogonga mwamba, huku Manuel Akanji wa Uswisi naye akikosa kwa kupiga juu ya lango.

Hata hivyo, Gregor Kobel aliibuka shujaa baada ya kuokoa penalti ya Cucho Hernandez kabla ya Ruben Vargas kufunga penalti ya ushindi na kuipeleka Uswisi robo fainali.

Nahodha wa Uswisi, Granit Xhaka, alisema kizazi cha sasa cha wachezaji wa nchi hiyo ni cha kipekee na kinaamini kuwa hata taifa dogo linaweza kufanya makubwa katika soka la dunia.

Kwa upande wa Colombia, mshambuliaji Luis Suarez alisema licha ya kuondolewa, timu hiyo imeonyesha kiwango kizuri katika mashindano hayo na anaamini uzoefu huo utakuwa chachu ya mafanikio makubwa siku zijazo.

Leave a Comment