×

Mnyika Avunja Ukimya: Afunguka Kusimamishwa kwa Viongozi, Fedha za Chadema – Video

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika.

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika, amesema uamuzi wa kuwasimamisha baadhi ya viongozi wa chama katika mikoa ya Morogoro na Tanga ulitokana na taarifa za ndani zilizokuwa zikifanyiwa kazi na uongozi wa chama.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 10, 2026 katika makao makuu ya CHADEMA jijini Dar es Salaam, Mnyika alisema chama kilipokea taarifa mapema kuwa kulikuwa na watu waliodaiwa kupewa fedha kwa lengo la kufanya mkutano na waandishi wa habari ili kuwachafua baadhi ya viongozi wa chama hicho.

Alisema baada ya kufuatilia taarifa hizo, uongozi wa chama ulichukua hatua kwa kuzingatia taratibu na kanuni za ndani, huku akisisitiza kuwa CHADEMA haitasita kuwawajibisha viongozi au wanachama watakaobainika kwenda kinyume na maadili na maslahi ya chama.

Fedha za CHADEMA ziko salama

Akizungumzia tuhuma kuhusu matumizi ya fedha za chama, Mnyika alisema fedha zote zinazochangwa kwa ajili ya CHADEMA ziko salama na matumizi yake yanafanyika kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.

Alifafanua kuwa fedha zinazopatikana kupitia kampeni ya Tonetone hulazimika kwanza kuingizwa kwenye akaunti ya benki kabla ya kutumika kwa shughuli mbalimbali za chama, ikiwemo ununuzi wa mafuta na mahitaji mengine ya uendeshaji.

Mnyika alisema wanaotoa tuhuma kuhusu matumizi ya fedha hizo hawafahamu utaratibu wa kifedha unaotumiwa na chama, akiongeza kuwa CHADEMA bado kinakabiliwa na uhitaji mkubwa wa fedha huku mapato yanayopatikana yakiwa hayakidhi mahitaji yake.

Aeleza kutokuwepo kwa Sugu

Mnyika pia alizungumzia kutokushiriki kwa Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi (Sugu), katika operesheni za chama zilizofanyika katika kanda yake.

Alisema Sugu alikuwa akiendelea na shughuli za chama katika Kanda ya Kati na aliiamini timu iliyokuwa ikiendesha operesheni Kanda ya Nyasa, iliyokuwa ikiongozwa na Mjumbe wa Kamati Kuu Godbless Lema pamoja na Salma Kasanzu, wakishirikiana na viongozi wengine wa kanda, akiwemo Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani, Boniface Jacob (Boniyai).

Katika hatua nyingine, Mnyika alisema Kamati Kuu ya CHADEMA, iliyokutana Juni 30, 2026 mjini Kigoma, imebaini kuwa Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2026/2027 haijaakisi hali halisi ya changamoto za maisha zinazowakabili Watanzania.

Kwa mujibu wa Mnyika, chama kinaamini bajeti hiyo haijajikita katika kuwainua wananchi kiuchumi, bali itaendelea kuwaacha wengi wakikabiliwa na ugumu wa maisha.

Alisema pia bajeti hiyo haijaweka mikakati ya kuongeza uwezo wa wananchi kununua bidhaa na huduma (purchasing power) wala kupunguza gharama za maisha.

Mnyika alihitimisha kwa kusema CHADEMA itaendelea kutoa maoni na mapendekezo yake kuhusu masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa maslahi ya wananchi na kuwataka wanachama kuendelea kuwa watulivu huku chama kikiendelea kushughulikia masuala yake ya ndani kwa mujibu wa katiba na kanuni zake.

Leave a Comment