

Dar es Salaam – Wengi wanamfahamu ChardTalent kupitia nyimbo zake za vichekesho na video zinazovuma mitandaoni, lakini nyuma ya mafanikio hayo kuna safari iliyojaa majaribu, kujifunza na kuthubutu kufanya jambo tofauti katika tasnia ya burudani nchini.
ChardTalent, ambaye jina lake halisi ni Mkasa Richard, alizaliwa Manyoni mkoani Singida na kukulia Dodoma. Alisomea Journalism and Mass Communication, na ingawa hakuhitimu, anasema elimu hiyo ilimjengea uwezo wa kuwasiliana kwa ufanisi na hadhira kupitia maudhui yake.
Badala ya kuchagua kuwa mwanamuziki au mchekeshaji pekee, aliamua kuunganisha vipaji vyake na kuanzisha mtindo alioupa jina la MuKi (Muziki wa Kiucheshi).
“Nilikuwa najiuliza kwa nini nichague muziki au comedy wakati naweza kufanya vyote kwa pamoja. Hapo ndipo nikaanza kujenga MuKi,” anasema.

Anakiri kuwa mwanzoni watu wengi walishangazwa na mtindo huo mpya. Ili kuuboresha, alijifunza kutoka kwa wasanii wa kimataifa akiwemo Ken Bláq wa Nigeria na Morgan Jay wa Marekani, huku akijenga utambulisho wake binafsi.
Hata hivyo, safari yake haikukosa changamoto. Moja ya nyakati ngumu zaidi ilikuwa wakati wa tamasha moja mkoani Njombe, ambapo mazingira hayakuwa rafiki kwa maonyesho ya vichekesho.
“Watu walikuwa wamelewa na walikuwa wananiambia nishuke jukwaani. Iliniuma sana na nikafikiria kuacha kabisa,” anakumbuka.
Baadaye alipata nafasi ya kutumbuiza katika tamasha kubwa jijini Dar es Salaam. Kabla hajapanda jukwaani, mchekeshaji Eliudi alimpa maneno yaliyobadili mtazamo wake.
“Panda mdogo wangu.”
Anasema maneno hayo yalimpa ujasiri mkubwa na tangu siku hiyo akaanza kujiamini zaidi jukwaani.
Kwa sasa, ChardTalent ni mmoja wa watumbuizaji wa Cheka Tu na amejenga ushawishi mkubwa mitandaoni akiwa na zaidi ya wafuasi milioni 1.1 kwenye TikTok, 562,000 kwenye Instagram na 428,000 kwenye Facebook. Pia ameshirikiana na kampuni mbalimbali zikiwemo Airtel Tanzania, National Lottery Tanzania, DStv Tanzania na Sendwave.
Mbali na muziki na vichekesho, ChardTalent anafahamika kwa uwezo wake wa kuigiza wahusika mbalimbali kwa kutumia lafudhi za Kimaasai, Kisukuma na Kimakonde.
“Bado nina ndoto nyingi. Nataka MuKi ikue na itambulike ndani na nje ya Tanzania. Kama kazi yangu itawafanya watu watabasamu na waamini ubunifu unaweza kuwa taaluma, nitafurahi sana,” anasema.