
Jeshi la Nigeria limetangaza kumkamata mwanamke raia wa Chad anayeshukiwa kuhusika katika usambazaji wa dawa za kulevya, pombe na bidhaa nyingine haramu kwa wapiganaji wa kundi la Boko Haram.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na msemaji wa Jeshi la Nigeria, Mohammed Goni, mwanamke huyo alikamatwa na wanajeshi wa Kikosi cha 3 cha Operesheni ya Pamoja Kaskazini Mashariki mwa Nigeria baada ya kupata taarifa za kijasusi zilizowawezesha kumfuatilia.
Mshukiwa huyo alikamatwa Julai 9 akiwa na kiasi kikubwa cha bidhaa zinazodaiwa kuwa zilikuwa zikisafirishwa kwenda kwa wapiganaji wa Boko Haram.
Jeshi limemtaja mshukiwa huyo kuwa ni Rachael Samuel, mwenye umri wa miaka 48, raia wa Chad.
Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa Samuel alikuwa akisafirisha bidhaa hizo kuelekea maeneo ya visiwa vya Ziwa Chad, eneo ambalo limekuwa likitajwa kuwa maficho ya baadhi ya makundi yenye silaha katika ukanda huo.
Miongoni mwa vitu vilivyokamatwa ni pamoja na mifuko saba ya bangi, pombe na bidhaa nyingine zinazodaiwa kuwa haramu ambazo jeshi linaamini zilikuwa zikielekezwa kwa wapiganaji wa Boko Haram.
Jeshi la Nigeria limesema uchunguzi zaidi unaendelea ili kubaini mtandao mzima unaoweza kuhusika katika usafirishaji huo na hatua zaidi zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria.