
Milango ya bahari (Maritime Chokepoints) ni njia nyembamba za maji zinazounganisha bahari au maeneo makubwa ya maji na kuruhusu meli kupita kutoka eneo moja kwenda jingine. Njia hizi zina nafasi kubwa katika biashara ya kimataifa, kwani sehemu kubwa ya mafuta, gesi na bidhaa mbalimbali husafirishwa kupitia maeneo hayo.
Kutokana na umuhimu wake, milango hii imekuwa kitovu cha biashara, diplomasia na hata migogoro ya kimataifa. Hizi ni baadhi ya milango muhimu zaidi duniani na mahali ilipo.
1. Strait of Hormuz
Mahali ilipo: Kati ya Iran upande wa kaskazini na Oman pamoja na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) upande wa kusini.
Strait of Hormuz ndiyo njia muhimu zaidi ya usafirishaji wa mafuta duniani. Inaunganisha Ghuba ya Uajemi na Ghuba ya Oman kabla ya kuingia Bahari ya Arabia na Bahari ya Hindi.
Kila siku, mamilioni ya mapipa ya mafuta husafirishwa kupitia njia hii kwenda Asia, Ulaya na Amerika. Kutokana na umuhimu wake, eneo hili limekuwa likikumbwa na mvutano wa kisiasa na kijeshi, hasa kati ya Iran na mataifa ya Magharibi.

2.Milango ya bahari Malacca
Mahali ilipo: Kati ya Malaysia, Indonesia na Singapore.
Njia hii inaunganisha Bahari ya Hindi na Bahari ya China Kusini na ni moja ya njia zenye shughuli nyingi zaidi za usafirishaji duniani.
Meli nyingi zinazobeba bidhaa kutoka Asia kwenda Ulaya, Afrika na Mashariki ya Kati hupitia hapa.

3. Suez Canal
Mahali ilipo: Misri (Egypt).
Mfereji wa Suez unaunganisha Bahari ya Mediterania na Bahari Nyekundu, na kutoa njia fupi kati ya Ulaya na Asia bila kulazimika kuzunguka Bara la Afrika.
Ni mojawapo ya miundombinu muhimu zaidi ya biashara duniani, ambapo maelfu ya meli hupita kila mwaka.

4. Panama Canal
Mahali ilipo: Panama, Amerika ya Kati.
Mfereji huu unaunganisha Bahari ya Atlantiki na Bahari ya Pasifiki, ukipunguza kwa kiasi kikubwa muda na gharama za safari za meli kati ya mabara hayo.
Panama Canal ni nguzo muhimu katika biashara ya kimataifa hasa kwa nchi za Amerika, Asia na Ulaya.

5. Bab el-Mandeb
Mahali ilipo: Kati ya Yemen upande wa Asia na Djibouti pamoja na Eritrea upande wa Afrika.
Mlango huu wa bahari unaunganisha Bahari Nyekundu na Ghuba ya Aden kabla ya kuingia Bahari ya Arabia.
Ni njia muhimu kwa meli zinazotumia Mfereji wa Suez, huku pia ukiwa eneo lenye umuhimu mkubwa wa kiusalama kutokana na migogoro inayowahi kutokea katika eneo hilo.

6. Bosporus
Mahali ilipo: Istanbul, Uturuki.
Bosporus ni mlango wa bahari unaounganisha Bahari Nyeusi na Bahari ya Marmara, na baadaye kuelekea Bahari ya Mediterania.
Mbali na kuwa njia muhimu ya biashara, Bosporus pia hutenganisha mabara mawili makubwa duniani – Ulaya na Asia.
Kwa nini milango hii ni muhimu?
Milango hii ya bahari ndiyo uti wa mgongo wa biashara ya kimataifa. Sehemu kubwa ya mafuta, gesi asilia, bidhaa za viwandani na malighafi hupitia katika njia hizi kila siku.
Endapo mojawapo ya njia hizi itafungwa kutokana na vita, migogoro au majanga ya asili, athari zake huonekana duniani kote kupitia kupanda kwa bei za mafuta, kuchelewa kwa usafirishaji wa bidhaa na kuongezeka kwa gharama za biashara.
Kwa sababu hiyo, mataifa makubwa duniani yanaendelea kuwekeza katika kulinda usalama wa milango hii ya bahari, huku pia yakitafuta njia mbadala za usafirishaji ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza pale njia mojawapo inapokumbwa na changamoto.