
Rais wa Marekani Donald Trump amesema Marekani inaweza kuchukua jukumu la kuusimamia na kuulinda Mlango wa Bahari wa Hormuz (Strait of Hormuz), akisisitiza kuwa mataifa yanayonufaika na njia hiyo yanapaswa kuilipa Marekani kwa huduma hiyo.
Akizungumza kwa njia ya simu katika kipindi cha Fox & Friends cha Fox News, Trump alisema Marekani itaendelea kulinda njia hiyo muhimu ya kimataifa kwa usafirishaji wa mafuta na gesi.
“Tutauweka salama Mlango wa Hormuz, na huenda tukawa tunausimamia. Tutakuwa walinzi wa mlango huo. Labda tutajiita ‘Guardian Angel of the Strait’,” alisema Trump.

Trump aliongeza kuwa Marekani haitafanya kazi hiyo bila malipo.
“Tutaulinda, na tutalipwa kwa kuulinda – fedha nyingi. Mataifa mengine ni tajiri sana, yako upande wetu, hivyo hayawezi kutarajia tufanye kazi hiyo bure,” alisema.
Kauli hiyo inakuja wakati Trump akiendelea kusisitiza kuwa vikosi vya Marekani vina udhibiti wa Mlango wa Hormuz tangu kuanza kwa vita kati ya Marekani, Israel na Iran.
Hata hivyo, Iran imeendelea kuonyesha uwezo wake wa kuathiri usalama wa njia hiyo muhimu kwa kutishia na wakati mwingine kushambulia meli zinazopita katika eneo hilo, hali ambayo imeendelea kuzua wasiwasi kuhusu usafirishaji wa mafuta na athari zake kwa uchumi wa dunia.