
KAMPUNI ya Oryx Gas Tanzania imezindua rasmi Kitabu cha Mwongozo wa Matumizi Salama ya Gesi ya LPG na wakati huohuo kusaini mkataba wa ushirikiano wa miaka mitatu na Chama cha Skauti Tanzania, hatua inayolenga kuimarisha elimu ya matumizi salama ya gesi ya kupikia kwa wananchi kupitia mtandao wa vijana wa Skauti nchini.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kitabu hicho na utiaji saini wa makubaliano hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Oryx Gas Tanzania, Benoit Araman, alisema mwongozo huo ni nyenzo muhimu ya kujifunzia na kufundishia matumizi sahihi ya gesi ya LPG, huku ushirikiano na Skauti ukilenga kuhakikisha elimu hiyo inawafikia Watanzania wengi zaidi.
Alisema kampuni inaamini kuwa pamoja na kuwajibika kwa wanahisa, wafanyakazi na Serikali, wananchi ndio wadau wake wakuu, hivyo imeamua kuwekeza katika elimu ya usalama ili kupunguza ajali zinazotokana na matumizi yasiyo sahihi ya gesi.

“Tunataka kuona Watanzania wengi zaidi wakitumia gesi ya LPG kwa usalama. Hatuwezi kuwafikia mamilioni ya watumiaji peke yetu, ndiyo maana tumeamua kushirikiana na Chama cha Skauti Tanzania chenye mtandao mkubwa wa vijana wanaoweza kuifikisha elimu hii kwa jamii,” alisema Araman.
Alieleza kuwa kupitia makubaliano hayo, Oryx Gas itawajengea uwezo wakufunzi wa Skauti kwa mfumo wa kumfundisha mkufunzi, ambao nao wataendelea kuwafundisha wananchi katika maeneo mbalimbali nchini kuhusu matumizi salama ya gesi ya LPG.
Aidha, alisema kitabu hicho, kilichoandaliwa kwa ushirikiano na Meneja wa Mafunzo wa Oryx Gas, Peter Ndomba, kitakuwa rejea muhimu kwa watumiaji wa gesi licha ya maendeleo ya teknolojia na matumizi ya mifumo ya kidijitali.
“Ni muhimu kuwa na nyenzo ambayo mtu anaweza kuishika mkononi, akaisoma mara kwa mara na kuirejea kila anapohitaji kujifunza matumizi salama ya gesi,” aliongeza.
Araman alitangaza kuwa kitabu hicho kitapatikana katika mfumo wa nakala zilizochapishwa pamoja na toleo la kidijitali ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Kwa upande wake, Peter Ndomba, ambaye ndiye mtunzi wa kitabu hicho, alisema wazo la kukiandika lilitokana na maono ya Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni baada ya kubaini umuhimu wa kuongeza elimu ya usalama sambamba na kampeni za kuhamasisha matumizi ya nishati safi.
Alisema mwongozo huo utawasaidia watumiaji kuelewa kwa kina namna salama ya kutumia gesi ya LPG, huku ukitarajiwa kutumika pia kama nyenzo ya kufundishia katika taasisi mbalimbali ikiwemo shule baada ya kukamilika kwa taratibu za kupata hatimiliki.
Naye Skauti Mkuu wa Tanzania, Rashid Mchatta, alisema ushirikiano huo ni mwanzo wa safari ya kuwajengea vijana maarifa, ujuzi na fursa zitakazochangia maendeleo ya taifa.
“Tutahakikisha ushirikiano huu unatekelezwa kwa umakini ili vijana wetu wawe mabalozi wa elimu ya matumizi salama ya gesi na kusaidia kupunguza ajali zinazotokana na matumizi yasiyo sahihi ya LPG,” alisema.
Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa Chama cha Skauti Tanzania, Abubakar Mtitu, alisema makubaliano hayo yanaendana na misingi ya Skauti ya kuitumikia jamii kwa kuwajengea vijana uwezo wa kushiriki katika kutatua changamoto zinazoikabili jamii.
Alisema Skauti itaendelea kutumia mtandao wake wa vijana kueneza elimu ya matumizi salama ya gesi ya LPG pamoja na kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa ajili ya kulinda afya za wananchi na mazingira.