×

Hal Williams Aaga Dunia, Aacha Urithi Mkubwa Hollywood

Mwigizaji mkongwe wa Marekani, Hal Williams, anayekumbukwa zaidi kwa nafasi yake ya Afisa “Smitty” Smith katika kipindi maarufu cha televisheni cha miaka ya 1970, “Sanford and Son”, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 91.

Kwa mujibu wa mwakilishi wake, Williams alifariki Jumatano asubuhi nyumbani kwake huko Rancho Mirage, California, kutokana na sababu za kawaida za kiafya zinazohusiana na umri.

Meneja wake, Zna Portlock Houston, amesema Williams alikuwa amerejea siku mbili kabla kutoka Ohio ambako alihudhuria mkusanyiko wa kumbukumbu za kipindi cha Sanford and Son pamoja na mwigizaji mwenzake Howard Platt, aliyekuwa akiigiza kama Afisa Howard “Hoppy” Hopkins.

Williams alianza safari yake ya televisheni mwaka 1972 baada ya kupata nafasi katika Sanford and Son, akishirikiana na waigizaji wakubwa akiwemo Redd Foxx, aliyekuwa akicheza nafasi ya Fred Sanford, na Demond Wilson, aliyekuwa Lamont Sanford.

Baadaye mwaka 1973, alipata nafasi nyingine kubwa katika kipindi maarufu cha “The Waltons” akicheza kama Harley Foster. Pia alijipatia umaarufu kupitia tamthilia ya vichekesho “227”, ambako aliigiza kama Lester Jenkins.

Katika maisha yake ya uigizaji, Williams alionekana pia katika vipindi mbalimbali vya televisheni kama “Good Times”, “Gunsmoke”, “Hill Street Blues”, “Magnum P.I.”, “Night Court” na “L.A. Law”.

Mbali na televisheni, Hal Williams pia alishiriki katika filamu mbalimbali ikiwemo “Hardcore”, “The Rookie”, “Percy & Thunder” na “Flight”.

Williams ameacha historia kubwa katika tasnia ya burudani baada ya zaidi ya miongo kadhaa ya kazi yake ya uigizaji.

Leave a Comment