×

Iran Yaionya Marekani, Yashambulia Mataifa Yanayohifadhi Vikosi Vyake

Mvutano wa kijeshi kati ya Iran na Marekani umeingia katika hatua mpya baada ya Iran kurusha makombora na ndege zisizo na rubani (droni) kuelekea Bahrain, Kuwait na Jordan, ikisema imelenga vituo vya kijeshi vya Marekani vilivyopo katika mataifa hayo.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Iran, mashambulizi hayo yalifanyika mapema Alhamisi ikiwa ni hatua ya kulipiza kisasi kufuatia mashambulizi mapya ya Marekani ndani ya Iran, yaliyolenga vituo vya ulinzi wa anga, mifumo ya makombora, vituo vya amri na maeneo ya kijeshi katika miji kadhaa ikiwemo Bandar Abbas na maeneo ya karibu na Tehran.

Jeshi la Jordan limesema lilifanikiwa kuyatungua makombora manane yaliyorushwa kuelekea nchini humo, huku Kuwait ikitangaza kuwa mifumo yake ya ulinzi wa anga ilizuia makombora manne na droni 21. Bahrain nayo iliwataka wakazi wake kutafuta maeneo salama baada ya ving’ora vya tahadhari kulia.

Iran imesema mashambulizi yake yalilenga vituo vya kijeshi vya Marekani, ikiwemo Ali Al-Salem Air Base nchini Kuwait na Sheikh Isa Air Base nchini Bahrain, pamoja na miundombinu ya mawasiliano na hifadhi ya mafuta inayotumiwa na jeshi la Marekani nchini Jordan.

Wakati huo huo, Jeshi la Marekani kupitia US Central Command (CENTCOM) limethibitisha kufanya mashambulizi mapya ndani ya Iran, likisema liliharibu vituo vya amri, mifumo ya ulinzi wa anga, uwezo wa makombora na droni pamoja na vifaa vya ufuatiliaji wa pwani vinavyohusishwa na usalama wa Mlango wa Hormuz.

Iran imesema watu zaidi ya 35 wamefariki dunia na zaidi ya 300 kujeruhiwa kutokana na mashambulizi ya Marekani yaliyofanyika katika siku za hivi karibuni.

Aidha, Marekani imeendelea kuimarisha vizuizi vya baharini dhidi ya Iran kwa kuzuia meli zinazodaiwa kuelekea bandari za Iran, hatua ambayo imeongeza hofu ya usumbufu wa usafirishaji wa mafuta duniani kupitia Mlango wa Hormuz, njia muhimu inayobeba karibu asilimia 20 ya mafuta na gesi ya dunia.

Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Bagher Qalibaf, amesema taifa hilo linaingia katika kile alichokiita “vita vya kulinda uhai wa taifa,” akionya kuwa Iran itaendelea kujibu kwa nguvu ikiwa mashambulizi ya Marekani yataendelea.

Kwa upande wake, Rais wa Marekani Donald Trump amesema bado anaamini Iran ipo tayari kwa mazungumzo ya kumaliza mzozo huo, licha ya mashambulizi yanayoendelea kati ya pande hizo mbili.

Mapigano hayo yameongeza hofu ya kuibuka kwa vita kubwa zaidi katika Mashariki ya Kati, huku mataifa mengi yakifuatilia kwa karibu hali inavyoendelea katika eneo la Ghuba ya Uajemi.

Leave a Comment