×

Mabingwa wa Dunia 2026 Kupewa Pete Maalum za Ubingwa Kwa Mara ya Kwanza

Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limeamua kuanzisha utamaduni mpya katika historia ya Kombe la Dunia kwa kuwazawadia mabingwa wa mashindano ya mwaka 2026 pete maalum za ubingwa.

Hatua hiyo ni mara ya kwanza kwa mabingwa wa Kombe la Dunia kupata pete kama kumbukumbu rasmi ya mafanikio yao, utamaduni ambao umekuwa ukifahamika zaidi katika michezo mikubwa nchini Marekani kama NFL na NBA, ambapo wachezaji na viongozi wa timu bingwa hupewa pete maalum baada ya kutwaa mataji.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, jumla ya pete 30 maalum zitatengenezwa kwa ajili ya timu itakayobeba Kombe la Dunia 2026, huku wachezaji na viongozi muhimu wa timu hiyo wakipewa kama kumbukumbu ya ushindi wao wa kihistoria.

Aidha, pete nyingine 1,996 zitatengenezwa na kuuzwa kwa mashabiki watakaotaka kumiliki kumbukumbu hiyo maalum ya michuano mikubwa zaidi ya soka duniani.

Kombe la Dunia 2026 litakuwa na historia ya kipekee kutokana na kuwa mara ya kwanza kushirikisha timu 48, huku likiwa mwenyeji wa pamoja katika nchi tatu za Amerika Kaskazini — Marekani, Canada na Mexico.

Hatua ya FIFA kutoa pete za ubingwa inaonekana kuwa njia ya kuongeza thamani ya kihistoria na kibiashara ya mashindano hayo, sambamba na kuipa timu itakayotwaa taji hilo kumbukumbu ya kipekee.

Leave a Comment