
Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Kigoma, imetupilia mbali shauri la kupinga uteuzi wa Makamishna wa Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Kijinai katika Matukio ya Ghasia za Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, inayojulikana kama Tume ya Jaji Lila.
Uamuzi huo umetolewa , Julai 17, 2026, na Jaji Wilbert Chuma, aliyekuwa akisikiliza shauri hilo lililofunguliwa na wanaharakati Bubelwa Ephraim Bubelwa na Joseph Daudi Mabugo, waliowakilishwa na mawakili Mpale Mpoki na Hekima Mwasipu.
Katika shauri hilo, walalamikaji walifungua maombi ya mapitio ya kimahakama (Judicial Review) dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji wa Mahakama ya Rufani Shaban Ally Lila, pamoja na makamishna wengine watatu ambao ni Majaji Wastaafu wa Mahakama Kuu, Gad John Mjemmas, Awadh Mohamed Bawazir na Aishieli Nelson Sumari.
Walidai kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, hakuwa na mamlaka ya kuunda tume hiyo mpya baada ya kukamilika kwa kazi ya Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, iliyoongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman.
Hata hivyo, Jaji Chuma alitupilia mbali hoja hizo akisema kuwa kwa mujibu wa Kifungu cha 3 cha Sheria ya Tume za Uchunguzi, Rais ana mamlaka ya kuunda Tume ya Uchunguzi.
Jaji huyo alieleza kuwa hatua za kuifanya tume hiyo kuwa halali kisheria bado hazijakamilika, kwani ni lazima kwanza itangazwe katika Gazeti la Serikali na makamishna wake waape viapo rasmi kabla ya kuanza kazi.
“Malalamiko haya kuhusu uhalali wa tume hii yamewasilishwa kabla ya wakati. Mahakama inaona maombi haya yamekosa mashiko na hivyo inayatupilia mbali,” alisema Jaji Chuma.
Tume ya Uchunguzi wa Kijinai katika Matukio ya Ghasia za Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 iliundwa na Rais Samia Suluhu Hassan kufuatia mapendekezo ya Tume ya Jaji Chande, ambayo iliwasilisha ripoti yake Aprili 23, 2026. Uteuzi wa Mwenyekiti na Makamishna wa tume hiyo ulitangazwa rasmi Mei 18, 2026.