
Pemba, Julai 16, 2026 – Airtel Tanzania imeendelea kutekeleza mkakati wake wa kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kuzindua duka la kisasa yani Smart Shop mpya katika Mkoa wa Kusini Pemba eneo la Chakechake, hatua inayolenga kuboresha upatikanaji wa huduma za mawasiliano na huduma za kifedha kidijitali pamoja na kuimarisha uzoefu wa wateja.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi huo, Meneja Biashara wa Airtel Tanzania, Bw. Gasper Ngowi, alisema uwekezaji huo unaakisi dhamira ya kampuni ya kuendelea kuwekeza katika miundombinu, teknolojia na huduma zinazowawezesha wananchi kupata huduma bora kwa urahisi zaidi.
“Sisi Airtel Tanzania tunaamini kuwa huduma bora huanza kwa kusikiliza mahitaji ya wateja na kuwafikia walipo. Ndiyo maana tunaendelea kuwekeza katika maduka ya kisasa, mifumo ya kidijitali, teknolojia na watu wetu ili kuhakikisha kila mteja anapata huduma ya haraka, sahihi na kwa ukaribu zaidi,” alisema Bw. Ngowi.
Alisema uzinduzi wa Smart Shop hiyo ni sehemu ya mkakati wa Airtel Kila Kona, unaolenga kuhakikisha huduma za Airtel zinapatikana karibu zaidi na wananchi, huku zikichangia kukuza ujumuishi wa kidijitali na uchumi jumuishi nchini.
Bw. Ngowi alisema Airtel Tanzania itaendelea kushirikiana na Serikali katika kuwekeza kwenye miundombinu ya mawasiliano inayochochea ukuaji wa biashara, kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuharakisha maendeleo ya uchumi wa kidijitali nchini.
Aliongeza kuwa Airtel Tanzania, ambayo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inamiliki asilimia 49 ya hisa zake, hivi karibuni ilikabidhi Serikali gawio la Shilingi bilioni 65.48, sambamba na kuendelea kuwekeza katika upanuzi wa mtandao na huduma za kidijitali nchini.
Kupitia Smart Shop hiyo, wananchi wa Pemba watapata huduma mbalimbali za Airtel katika eneo moja, ikiwemo usajili wa laini mpya, kubadilisha wa kadi ya SIM, huduma za Airtel Money, intaneti, ununuzi wa simu janja na vifaa vya mawasiliano pamoja na huduma za ushauri kutoka kwa wataalamu wa huduma kwa wateja.
Bw. Ngowi alisema ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika Kisiwa cha Pemba, unaochochewa na maendeleo ya sekta ya utalii, uchumi wa buluu, maboresho ya miundombinu na kuongezeka kwa shughuli za biashara, umeongeza mahitaji ya huduma za mawasiliano na huduma za kifedha kidijitali, na hivyo kuifanya Pemba kuwa eneo muhimu kwa uwekezaji wa Airtel Tanzania.
Alisisitiza kuwa lengo la Airtel ni kuhakikisha kila mteja anayefika katika duka hilo anapata suluhisho la mahitaji yake kwa haraka na uzoefu unaokidhi viwango vya kimataifa vya huduma kwa wateja.
Uzinduzi wa duka la kisasa la Airtel Kisiwani Pemba unaendelea kuimarisha utekelezaji wa dhamira ya Airtel Tanzania ya kuunganisha Watanzania kupitia huduma za kisasa, ujumuishi wa kidijitali na kusogeza huduma karibu zaidi na jamii kupitia mkakati wa Airtel Kila Kona.