
Katika kuendelea kusikilizwa kwa shauri linalomhusu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, katika Mahakama Kuu, Lissu aliendelea kumhoji Mkuu wa Gereza Kuu la Ukonga, Andrew Hassan, kuhusu malalamiko ya mawakili wake kunyimwa haki ya kuonana naye kwa faragha na madai ya mawasiliano yao kufuatiliwa wanapomtembelea gerezani.
Kupitia maswali ya dodoso, shahidi alikubali kuwa Kanuni za Magereza zinatambua haki ya wafungwa kutembelewa pamoja na haki ya mawakili kuwatembelea wateja wao.
Lissu aliendelea kuhoji kuhusu utaratibu wa uangalizi kwa wafungwa wa adhabu ya kifo, ambapo shahidi alikiri kuwa sheria inawataka wasimamiwe na askari wasiopungua watatu, lakini akasema hakuna kanuni inayoweka utaratibu huo kwa mahabusu.

Pia alikubaliana kuwa sheria na kanuni za magereza hazitambui kundi la “watuhumiwa wa kisiasa,” bali zinatambua makundi ya wafungwa wa kawaida, wenye umri mdogo na wa mara ya kwanza.
Katika hoja ya haki ya mawakili kuonana na wateja wao, shahidi alisema askari wanaweza kuwaona wakili na mteja wake lakini hawapaswi kusikiliza mazungumzo yao.
Hata hivyo, alikubali kuwa aliwaandikia maofisa wake maelekezo ya “kusimamia kwa karibu” mazungumzo ya mawakili waliokuwa wakimtembelea Lissu, akieleza kuwa lengo lilikuwa kuhakikisha utaratibu unafuatwa na si kusikiliza mazungumzo, ingawa hakuwahi kuandika maelekezo yanayokataza askari kusikiliza mazungumzo hayo.
Shahidi pia alithibitisha alimkuta Lissu akiwa katika eneo la Special Wing alipohamishiwa Gereza la Ukonga, pamoja na kuwepo kwa orodha ya mawakili walioruhusiwa kumtembelea.
Mwishoni mwa dodoso, alikanusha kumpiga marufuku viongozi wa CHADEMA kumtembelea Lissu, huku akieleza kuwa hawezi kuruhusu suala hilo kwa sasa kwa kuwa bado liko mbele ya Mahakama. Mahakama imeahirisha shauri hilo hadi kesho ili kuendelea na maswali ya dodoso.