
Washington, D.C. – Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth, amesema gharama za vita dhidi ya Iran zimefikia dola bilioni 37.5 (Shilingi trilioni 101.25 za Tanzania), zikiongezeka kutoka makadirio ya awali ya karibu dola bilioni 29 yaliyotolewa katikati ya Mei.
Akizungumza mbele ya Kamati ya Bajeti ya Seneti, Hegseth alitetea ombi la Pentagon la kuidhinishiwa takribani dola bilioni 67 ( Tsh trilioni 180.9) za ziada ili kugharamia operesheni za kijeshi dhidi ya Iran hadi mwisho wa mwezi Septemba.
Hegseth, akishirikiana na Mwenyekiti wa Wakuu wa Majeshi ya Marekani, Jenerali Dan Caine, waliwaambia maseneta kuwa fedha hizo ni za haraka na muhimu ili kuhakikisha shughuli za kijeshi zinaendelea bila kukwama.
Hata hivyo, Seneta wa Chama cha Democratic, Jeanne Shaheen, alipinga ombi hilo akisema Pentagon bado ina takribani dola bilioni 75 (Tsh trilioni 202.5) ambazo hazijatumika.
Alihoji kwa nini serikali inaomba walipa kodi kubeba gharama za vita ambavyo, kwa mujibu wake, havina uungwaji mkono mkubwa wa Wamarekani, badala ya kutumia fedha ambazo tayari zimetengwa lakini hazijatumika.
Kwa kujibu hoja hiyo, Hegseth alisema fedha hizo tayari zimepangwa kutekeleza vipaumbele vingine vya Rais Donald Trump, ikiwemo mradi wa “Golden Dome for America”, maendeleo ya silaha za hypersonic na uwekezaji mwingine wa kijeshi.
Aidha, ombi hilo la dola bilioni 67 halijumuishi gharama zitakazohitajika kujenga upya vituo vya kijeshi vya Marekani vilivyoko Mashariki ya Kati.
Wakati wa kikao hicho, wabunge kutoka vyama vyote viwili walitaka serikali kutoa maelezo zaidi kuhusu mkakati wa Marekani katika vita hivyo.
Seneta wa Republican, John Kennedy, alisema Congress inahitaji majibu ya wazi kuhusu mustakabali wa operesheni hizo, akitaka kufahamu nini kingetokea iwapo Marekani ingeondoa uwepo wake katika Mlango Bahari wa Hormuz, njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani.
Hata hivyo, Hegseth na Jenerali Caine hawakutoa maelezo ya kina kuhusu uwezekano wa Iran kuweka tozo kwa meli zinazopita katika eneo hilo.