
Mvutano wa kijeshi kati ya Marekani na Iran umeendelea kuongezeka baada ya Iran kudai kushambulia kambi za kijeshi za Marekani zilizopo Jordan na Bahrain, huku Bahrain ikiwasha ving’ora vya tahadhari mapema Ijumaa na kuwaagiza wananchi wake kujikinga.
Mashambulizi hayo yamekuja saa chache baada ya Jeshi la Marekani kutangaza kukamilisha usiku wa 13 mfululizo wa mashambulizi dhidi ya Iran, yakilenga kudhoofisha uwezo wa Tehran kutishia usafiri wa meli za kibiashara katika eneo la Mlango wa Hormuz.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali ya Iran, jeshi la nchi hiyo lililenga Kambi ya Al-Azraq nchini Jordan pamoja na Kambi ya Sheikh Isa nchini Bahrain. Mataifa ya Ghuba yamekuwa yakikumbwa na mashambulizi ya mara kwa mara huku mzozo kati ya Marekani na Iran ukiendelea kushika kasi.

Wakati huohuo, waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran nchini Yemen walitangaza kuwa walilenga meli mbili za mafuta za Saudi Arabia katika Bahari ya Shamu (Red Sea), hatua inayoongeza hofu ya kusambaa kwa vita katika eneo hilo.
Houthi pia wametishia kufunga Mlango wa Bab el-Mandeb, njia nyingine muhimu ya biashara ya kimataifa inayounganisha Bahari ya Shamu na Ghuba ya Aden. Takribani asilimia 12 ya biashara ya dunia na robo ya usafirishaji wa makontena hupitia eneo hilo kuelekea au kutoka Mfereji wa Suez.
Rais wa Marekani Donald Trump ameonya kuwa Houthi watakabiliwa na “adhabu kubwa ya kijeshi” ikiwa wataendelea kushambulia meli zinazopita katika eneo hilo.
Katika upande mwingine, milipuko iliripotiwa kwenye Kisiwa cha Qeshm nchini Iran pamoja na maeneo ya Ahvaz, ambapo vyombo vya habari vya serikali ya Iran vilisema watu wanne waliuawa na watano kujeruhiwa kufuatia shambulio la kombora la Marekani.

Kutokana na hali hiyo, bei ya mafuta ghafi aina ya Brent imepanda kwa zaidi ya asilimia sita na kufikia karibu dola 100 kwa pipa, kiwango cha juu zaidi katika miezi ya hivi karibuni, huku hofu ya kuvurugika kwa usambazaji wa mafuta duniani ikiendelea kuongezeka.
Iran imeendelea kusisitiza kuwa ina haki ya kusimamia shughuli za usafiri katika Mlango wa Hormuz na hata kutoza ada kwa meli zinazopita, jambo ambalo limepingwa na Marekani.
Trump pia alisema fedha za Iran zilizozuiliwa na Marekani zinaweza kutumika kugharamia uharibifu wa meli uliojitokeza kutokana na vita hivyo. Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, alikosoa kauli hiyo akisema hatua ya kunyakua mali za mataifa mengine inaweza kuhatarisha usalama wa mali za nchi zote duniani.