×

Stanbic na Visa Waandika Historia, Matumizi ya Kadi Yaruka kwa Asilimia 201

Dar es Salaam, Tanzania – 23 Julai 2026: Wakati Tanzania ikipiga hatua kubwa kuelekea uchumi usiotegemea fedha taslimu, Benki ya Stanbic, kwa ushirikiano na Visa, imehitimisha kampeni iliyoleta ongezeko kubwa la malipo salama ya kidijitali yanayovuka mipaka — hatua inayothibitisha dhamira ya pande zote mbili katika kuunga mkono ajenda pana ya taifa ya malipo ya kidijitali na ujumuishwaji wa kifedha.

Matokeo yanaonyesha mabadiliko makubwa katika tabia za wateja. Katika kipindi cha kampeni, matumizi ya kadi yaliongezeka kwa asilimia 113 kwa idadi ya miamala na asilimia 201 kwa thamani, huku uanzishaji wa matumizi ya kadi (card activation) ukiongezeka kwa asilimia 3,082 kwa idadi ya miamala na asilimia 449 kwa thamani — ishara wazi ya ujasiri wa wateja unaokua kwa kasi katika malipo ya kidijitali yanayovuka mipaka.

Kampeni hii inakuja katika kipindi muhimu kwa Tanzania. Huku Serikali sasa ikitaka matumizi ya malipo ya kidijitali katika sekta muhimu za uchumi, na Mfumo wa Kitaifa wa Ujumuishwaji wa Kifedha (2023–2028) ukiendeleza upatikanaji mpana wa huduma za kifedha zenye gharama nafuu, mahitaji ya njia za malipo zinazoaminika na zinazokubalika kimataifa yamekuwa makubwa kuliko wakati wowote. Kampeni ya Stanbic na Visa ya malipo yanayovuka mipaka iliundwa kukidhi wakati huu — ikiwapa wateja ujasiri wa kufanya miamala kwa usalama nje ya mipaka ya Tanzania.

Ikilenga wateja Binafsi na Maalum (Personal na Private Banking) wa Stanbic, kampeni ilihamasisha urahisi, usalama na ukubalifu wa kimataifa wa Kadi za Stanbic Visa kwa ajili ya safari za kimataifa, ununuzi mtandaoni, malipo ya elimu na miamala ya kibiashara. Iliunganisha mawasiliano ya moja kwa moja na wateja pamoja na elimu ya vitendo kuhusu faida za kuhama kutoka fedha taslimu kwenda malipo salama ya kidijitali — ikiwasaidia wateja kuelewa siyo tu jinsi ya kufanya miamala inayovuka mipaka, bali pia kwa nini kufanya hivyo kidijitali ni salama na rahisi zaidi.

Akizungumzia kampeni hiyo, Emmanuel Mahodanga, Mkuu wa Kitengo cha wateja Binafsi, Benki ya Stanbic, alisema matokeo haya yanaakisi dhamira ya pamoja inayovuka mipaka ya huduma za kibenki.

“Takwimu hizi zinatuonyesha kuwa Watanzania wako tayari kukumbatia malipo salama ya kidijitali — na ushirikiano wetu na Visa ni zaidi ya kutoa kadi; ni kuhusu kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali uliounganishwa,” alisema Mahodanga. “Wakati nchi ikiharakisha kuelekea malipo yasiyotumia fedha taslimu, jukumu letu ni kuwapa wateja njia salama zinazokubalika kimataifa wanazoweza kuziamini, wawe wanasafiri, wanasoma nje ya nchi au wanafanya biashara ya kimataifa. Kila mteja anayechagua kufanya miamala kidijitali anasaidia kujenga mfumo wa kifedha jumuishi na wa kisasa zaidi kwa Tanzania.”

Akisisitiza dhamira hiyo, Victor Makere, Meneja Mkazi, Visa Tanzania, alisema ushirikiano huu unaunga mkono mabadiliko mapana ya kidijitali ya taifa.

“Katika Visa, tunajivunia kushirikiana na Benki ya Stanbic katika kuendeleza malipo salama na yenye ufanisi ya kidijitali katika kipindi ambacho Tanzania inapiga hatua za kweli kuelekea uchumi usiotumia fedha taslimu,” alisema Makere. “Ukuaji wa kiwango hiki unaonyesha kile ambacho ushirikiano imara unaweza kufanikisha katika kujenga ujasiri wa kila siku ambao wateja wanauhitaji ili kufanya miamala inayovuka mipaka, huku ukiunga mkono lengo la taifa la Tanzania ya kidijitali na jumuishi zaidi kifedha. Tunatarajia kuimarisha zaidi ushirikiano wetu na Stanbic ili kuharakisha biashara ya kidijitali na kuwaletea wateja thamani kubwa zaidi.”

Kadi za Stanbic Visa zinawapa wateja njia za malipo salama, rahisi na zinazokubalika kimataifa, zikiwezesha miamala yenye ufanisi katika mamilioni ya wafanyabiashara duniani kote. Wawe wanasafiri, wanasoma nje ya nchi, wananunua mtandaoni au wanafanya malipo ya kibiashara ya kimataifa, wamiliki wa kadi wanaweza kufanya miamala kwa ujasiri popote ambapo Visa inakubalika, wakisaidiwa na vipengele vya usalama vilivyoimarishwa na fursa za safari, mtindo wa maisha na ofa mbalimbali za wafanyabiashara.

Kwa kuangalia mbele, Benki ya Stanbic na Visa wataendelea kuimarisha ushirikiano wao ili kupanua matumizi ya malipo ya kidijitali nchini Tanzania. Maeneo yaliyopangwa ni pamoja na kupanua elimu kwa wateja kuhusu malipo ya kimataifa na ya kidijitali, kuongeza upatikanaji wa zawadi za kimataifa na ofa za wafanyabiashara za Visa, na kutumia takwimu na uchambuzi ili kutoa huduma binafsi zinazolingana zaidi na mahitaji ya wateja.

Jitihada hizi zinaunga mkono dhamira ya Benki ya Stanbic ya kutoa suluhisho bunifu za kibenki zinazokidhi mahitaji yanayobadilika ya wateja, huku zikichangia mpito wa Tanzania kuelekea uchumi wa kidijitali, uliounganishwa na jumuishi zaidi kifedha.

Leave a Comment