
Wafanyabiashara wa Soko la Mawenzi mkoani Morogoro wamegoma kufungua biashara zao wakishinikiza Serikali kupunguza kodi ya pango la vizimba, wakidai kiwango cha sasa ni kikubwa na kinawaathiri kiuchumi.
Wafanyabiashara hao wamesema pamoja na kutozwa kodi kubwa, soko hilo bado lina miundombinu duni, hali inayosababisha wateja wengi kulikwepa na hivyo kupunguza mapato yao.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala, amefika katika soko hilo na kusikiliza malalamiko ya wafanyabiashara hao. Ameahidi kuyafanyia kazi changamoto walizozieleza, jambo lililowafanya wafanyabiashara kukubaliana kwa pamoja kuendelea na shughuli zao za biashara huku wakisubiri utekelezaji wa ahadi hizo.