×

Mwanaume Ashitakiwa Kwa Mauaji ya Mpenzi Wake, Apewa Dhamana ya Bilioni 3.2, Apiga Simu Polisi

Mwanaume, Kyle Collins mwenye umri wa miaka 37 anayeshtakiwa kwa mauaji ya mpenzi wake.

ARIZONA, Marekani – Mwanaume mmoja nchini Marekani anayeshtakiwa kwa mauaji ya mpenzi wake anakabiliwa na mashtaka ya mauaji na utekaji, baada ya mwanamke huyo kukutwa amefariki ndani ya nyumba waliyokuwa wakiishi pamoja.

Mwanaume huyo, Kyle Collins mwenye umri wa miaka 37, awali alipiga simu ya dharura 911 akidai kuwa amemkuta mpenzi wake, Cierra Tellez (36), akiwa hajitambui katika nyumba yao iliyopo mjini Mesa, Arizona.

Kwa mujibu wa mamlaka, polisi na wahudumu wa dharura walifika eneo hilo baada ya taarifa ya tukio la kiafya kutolewa Julai 21, 2026, lakini walimkuta Tellez akiwa amefariki huku akiwa na majeraha makubwa.

Baada ya uchunguzi wa awali, polisi walibaini kuwa kulikuwa na sababu za msingi za kumhusisha Collins na tukio hilo, na alikamatwa Julai 24, 2026 kwa tuhuma za mauaji ya daraja la kwanza na utekaji.

Katika kesi ya kwanza mahakamani, mwendesha mashtaka alisema tukio hilo lilikuwa la kikatili na la kutisha, huku akimtaja Collins kuwa ni mtu hatari kwa jamii.

“Tunaamini Bw. Collins ni mtu hatari sana,” alisema mwendesha mashtaka wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo.

Collins kwa sasa  yupo nje kwa dhamana ya dola za Marekani 1,250,500 (Bilioni 3.2 za Tanzania).

Jirani yao kupitia televisheni ya AZ amesema kuwa alishangazwa na kifo cha Tellez, akisema usiku uliotangulia alikuwa amekutana na Collins na hakukuwa na dalili zozote za tatizo.

Hata hivyo, jirani huyo alisema asubuhi ya tukio alimwona Collins akiwa amekasirika sana na akamweleza kuwa alikuwa amegombana na mpenzi wake.

Kwa mujibu wa taarifa za waendesha mashtaka, mwajiri wa Collins alisema hakufika kazini siku hiyo licha ya kudai kuwa alikuwa anaelekea kazini.

Uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea, huku haijafahamika mara moja kama Collins ana wakili anayemuwakilisha katika kesi hiyo.

Leave a Comment