
Mtengeneza maudhui wa mtandaoni (YouTuber) anayejulikana kwa kushiriki maudhui kuhusu manukato, Philip Carter (30), amefunguliwa mashtaka nchini Marekani kwa tuhuma za kuendesha mpango wa ulaghai uliodaiwa kumuingizia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Sheriff wa Kaunti ya Cook, Illinois, Carter anadaiwa kuagiza manukato ya kifahari yenye thamani ya maelfu ya dola kupitia mtandao. Baada ya kuyapokea, alidaiwa kuyaondoa kwenye vifungashio vyake na kuweka udongo wa kufinyanga (modeling clay) au chupa zilizokwisha kutumika, kisha kuvifunga upya kwa ustadi na kuvirudisha kwa wauzaji ili apate kurejeshewa fedha.
Uchunguzi ulianza mwezi Machi baada ya kampuni ya Nordstrom kuripoti kupokea manukato yaliyokuwa yamebadilishwa kupitia huduma ya posta. Polisi walizindua operesheni iliyopewa jina la “Operation Eau de Fraud”, na baada ya kuchunguza rekodi za kifedha, usafirishaji pamoja na matumizi ya mtandao, walimtambua Carter kama mtuhumiwa mkuu.
Mnamo Julai 22, maafisa walivamia nyumba yake jijini Chicago na kumkamata. Wakati wa upekuzi, walidai kukuta manukato 714 yenye thamani inayokadiriwa kufikia dola 250,000 (Sawa na Tsh 658,660,170.00), pamoja na masanduku yaliyokuwa tayari kwa ajili ya kurejeshwa, vifurushi vilivyokuwa na udongo badala ya manukato, vifaa vya kufungashia, gundi na kifaa cha kutoa joto (heat gun).
Uchunguzi pia uliwaongoza polisi kwenye akaunti ya YouTube ya Carter, ambapo alikuwa akionyesha hadharani mkusanyiko mkubwa wa manukato ya kifahari.
Carter ameshtakiwa kwa makosa matatu ya udanganyifu kupitia huduma za posta (mail fraud) pamoja na makosa matatu ya wizi kwa njia ya udanganyifu. Kesi yake inaendelea mahakamani, na kwa mujibu wa sheria, ataendelea kuchukuliwa kuwa hana hatia hadi mahakama itakapotoa uamuzi wa mwisho.