
Picha na video za ndege ya kifahari inayofahamika kwa jina la Royal Wings zimeendelea kusambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii, huku zikivutia mamilioni ya watu kutokana na muonekano wake wa kipekee unaofanana na kasri la kifalme linaloruka angani.
Kwa mujibu wa maelezo yanayosambazwa mtandaoni, ndege hiyo inadaiwa kuwa na thamani ya takribani dola bilioni 1.9 (takribani Shilingi za Tanzania trilioni 5.1) na imeundwa kwa ajili ya watu wa familia za kifalme pamoja na matajiri wakubwa duniani.
Inaelezwa kuwa ndani yake kuna vyumba vya kifahari, sebule binafsi, maeneo ya burudani, vyumba vya mikutano, sehemu za kupumzikia na mapambo ya marumaru, dhahabu na mawe ya thamani.

Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na vyombo mbalimbali vya ukaguzi wa taarifa umeonyesha kuwa hakuna ushahidi rasmi unaothibitisha kuwapo kwa ndege hiyo kama inavyodaiwa.
Hakuna kampuni ya utengenezaji wa ndege, shirika la anga wala mmiliki aliyewahi kutangaza mradi wa ndege hiyo yenye thamani na muundo huo.
Vyanzo vya ukaguzi vinaeleza kuwa picha na video nyingi zinazohusishwa na Royal Wings zinaonyesha dalili za kutengenezwa kwa kutumia teknolojia ya akili bandia (AI).

Wataalamu wa sekta ya anga pia wameeleza kuwa baadhi ya vipengele vinavyoonekana kwenye picha hizo havilingani na kanuni za uhandisi wa ndege zinazoweza kufanya safari salama angani.
Ingawa duniani zipo ndege nyingi za kifahari zinazomilikiwa na wafalme, marais na mabilionea, hadi sasa hakuna taarifa rasmi inayothibitisha uwepo wa ndege inayoitwa Royal Wings yenye thamani ya dola bilioni 1.9.
Kutokana na hali hiyo, simulizi la Royal Wings linaonekana kuwa ni ubunifu wa kidijitali uliotengenezwa kwa kutumia AI kwa ajili ya burudani na kuvutia watazamaji, badala ya kuwa mradi halisi wa usafiri wa anga.









