
Jeshi la Polisi nchini limetangaza kuondoa zuio la mikutano ya hadhara lililokuwa limewekwa awali, likisema hali ya usalama nchini kwa sasa ni shwari na inaruhusu shughuli hizo kuendelea kufanyika.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, uamuzi huo umefikiwa baada ya tathmini ya hali ya usalama kubaini kuwa mazingira yaliyopo yanaruhusu mikutano ya hadhara kufanyika kwa utulivu.
Misime amesema awali Jeshi la Polisi lilikuwa likiwashauri waandaaji wa mikutano kuiahirisha kutokana na hali ya kiusalama iliyokuwepo wakati huo, kwa lengo la kulinda usalama wa wananchi na mali zao.
Ameeleza kuwa kuanzia sasa, waandaaji wa mikutano ya hadhara wanapaswa kuendelea kuwasilisha taarifa za nia ya kufanya mikutano hiyo kwa Wakuu wa Polisi wa Wilaya husika, kwa mujibu wa sheria na taratibu zinazotumika.
Aidha, Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuendelea kushirikiana nalo kwa kutoa taarifa kuhusu viashiria vya uhalifu au mipango yoyote ya kutenda vitendo vya kihalifu ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa.
Jeshi hilo limesisitiza kuwa amani na usalama ni nguzo muhimu katika kuhakikisha shughuli za kisiasa, kijamii na kiuchumi zinaendelea kwa utulivu na kuchangia maendeleo ya taifa.
