×

WhatsApp Yazindua Mfumo Mpya wa Simu Unaorahisisha Mawasiliano

WhatsApp imetangaza maboresho mapya katika huduma zake za simu, ikileta vipengele vipya vitano vinavyolenga kuboresha mawasiliano ya watumiaji, ikiwemo uwezo wa kupiga na kupokea simu kupitia WhatsApp Web pamoja na kuboresha ubora wa sauti.

Kwa mujibu wa WhatsApp, maboresho hayo yanalenga kuwafanya watumiaji waweze kutumia huduma ya simu kwa urahisi zaidi wakiwa kwenye simu zao, kompyuta au wakibadilisha vifaa bila kukatisha mawasiliano.

Moja ya maboresho makubwa ni kupiga simu kupitia WhatsApp Web, ambapo watumiaji sasa wataweza kupiga na kupokea simu za sauti na video moja kwa moja kupitia kivinjari bila kulazimika kupakua programu. Huduma hiyo itafanya kazi kwa mazungumzo ya mtu mmoja mmoja au kwenye vikundi.

Watumiaji pia wataweza kutumia baadhi ya vipengele vilivyopo kwenye vifaa vingine kama kushirikiana skrini (screen sharing), kutuma miitikio (reactions) pamoja na sehemu maalum ya Calls tab itakayowasaidia kuona historia ya simu zao.

WhatsApp imesema simu zinazopigwa kupitia web zitaendelea kuwa na ulinzi wa end-to-end encryption, hazitakuwa na kikomo cha muda na zitakuwa bure.

Mbali na simu kupitia web, maboresho mengine mapya ni pamoja na:

  • Call Transfer: Kuruhusu mtumiaji kuhamisha simu inayoendelea kutoka kifaa kimoja kwenda kingine bila kukata mawasiliano.
  • Waiting Room: Kuwezesha wamiliki wa simu za vikundi kudhibiti wanaojiunga kwa kuwapa ruhusa kabla ya kuingia.
  • QuickHD: Kuboresha ubora wa video kwa kuwezesha matumizi ya picha za kiwango cha juu (HD) tangu mwanzo wa simu.
  • Noise Suppression: Kupunguza kelele za mazingira ili sauti iwe wazi zaidi hata mtumiaji akiwa sehemu yenye vurugu au kelele.

WhatsApp imesema vipengele hivyo vitaanza kupatikana kwa watumiaji hatua kwa hatua na vitakuwa vinapatikana kwa kila mtu katika kipindi kijacho.

Leave a Comment