×

CPA Tito Kitalika: Heche Hahusiki na Mfumo wa Fedha wa Chadema, Tuhuma Zipuuzwe – Video

Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo- CHADEMA, CPA Tito Kitalika amesema tuhuma wanazotoa watu kwamba Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, John Heche amekula fedha za tonetone ni za kupuuzwa.

Akizungumza leo Julai 31, 2026 katika kipindi cha Front Page kinachorushwa kila siku za Jumatatu hadi Ijumaa saa 2.30 asubuhi mpaka saa 4 asubuhi kwenye kituo cha televisheni cha Global Tvonline na +255 Global Radio mkurugenzi huyo alisema Heche hahusiki chochote kwenye mfumo wa kupokea au kutoa fedha wa Chadema.

“Makamu Mwenyekiti hahusiki chochote kwenye kutoa fedha za chama kwa sababu watu wanaosaini cheki ili fedha zitoke benki hayumo.

Mwenyekiti wa Taifa yupo lakini Tundu Lissu tangu achaguliwe hajawahi kutia Saini cheki yoyote ili fedha zitoke licha ya kuongoza chama kwa miezi mitatu tu kisha wakampeleka jela, hivyo wanaosema Heche amekula fedha za michango wanapaswa kupuuzwa kwa sababu tunajua lengo lao.

“Tunajua lengo lao wao wanatumika ili kukishinikiza chama kiingie kwenye maridhiano. Sisi Chadema tumeshasema hatuwezi kuingia kwenye maridhiano mpaka mwenyekiti wetu aachiiwe huru na msimamizi wa maridhiano atoke nje, huo ndio msimamo wa chama,” amesema CPA Tito Kitalika.

Alipoulizwa sababu ya baadhi ya wanachama wao kudai uchunguzi ufanyike CPA Tito Kitalika amesema hawawezi kushughulikia hilo jambo ambalo halina ukweli wowote na kuacha mambo ya msingi wanayoyapambania kama vile kushinikiza Lissu aachiwe huru na madai ya Katiba mpya.

CPA Tito Kitalika amesema wengi wanaozusha madai hayo wanatumika na wana ushahidi kwamba kuna fungu la fedha limetoka ili kushinikiza chama kiingie kwenye maridhiano” Wengi wanaoitisha mikutano na waandishi wa habari tunawajua.

Hawana uwezo wa kuitisha mikutano hiyo na kutoa shilingi milioni mbili kwa ajili ya mikutano” alidai kiongozi huyo.

Aliwahimiza wana Chadema kuchangia chama chao huku akisisitiza kuwa ana Imani kwamba wengi wana mapenzi na chama hicho kwa kuwa huwa kinawapigania katika mambo mbalimbali ambayo chama tawala kimeshindwa kuyafanya tangu tupate uhuru.

Leave a Comment