
Mwanamke aliyekuwa mwanajeshi wa Jeshi la Wanamaji la Uingereza (Royal Navy), Sian Dowsett (25), amehukumiwa kifungo cha miezi 18 katika gereza la kijeshi baada ya kupatikana na hatia ya kuwafanyia unyanyasaji wa kijinsia wenzake wanne akiwa kazini ndani ya meli ya kivita HMS Dauntless.
Mahakama ya kijeshi ilielezwa kuwa Dowsett aliwafanyia vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia wanajeshi wa kiume na wa kike katika matukio tofauti. Miongoni mwa vitendo vilivyotajwa ni kuwagusa sehemu za siri baadhi ya wanaume bila ridhaa yao, kuwashika na kuwabembeleza kwa namna isiyofaa, pamoja na kutoa kauli zenye maudhui ya kingono.

Kwa upande wa wanawake, mahakama ilisikiliza ushahidi ukieleza kuwa aliwagusa sehemu za mwili bila idhini yao, ikiwemo kupiga makalio na kushika matiti huku akitoa maneno yenye maudhui ya kingono.
Waendesha mashtaka walidai kuwa Dowsett aliwalenga zaidi wanajeshi wapya, akiamini kuwa wasingeweza kutoa taarifa dhidi yake kutokana na hadhi yao na mazingira ya kazi.

Jaji wa mahakama ya kijeshi alimwelezea Dowsett kuwa alikuwa akiwatisha na kuwanyanyasa wenzake, akisisitiza kuwa vitendo vyake vilikiuka maadili na nidhamu ya jeshi.
Baada ya kutiwa hatiani, alifukuzwa rasmi kutoka Jeshi la Wanamaji la Uingereza pamoja na kuhukumiwa kifungo cha miezi 18 gerezani.
Kesi hiyo imeibua mjadala kuhusu umuhimu wa kuhakikisha mazingira ya kazi yanakuwa salama kwa wote, bila kujali jinsia, na kusisitiza kuwa tuhuma za unyanyasaji wa kijinsia zinapaswa kuchunguzwa na kushughulikiwa kwa uzito sawa kwa wahusika wote.