×

Trump Atangaza Kusimamisha Mashambulizi Mapya dhidi ya Iran

Rais wa Marekani, Donald Trump, ametangaza kuwa ameamua kusitisha kwa muda mashambulizi mapya ya kijeshi dhidi ya Iran, akisema hatua hiyo inalenga kutoa nafasi kwa juhudi za kidiplomasia zinazolenga kumaliza vita vilivyoendelea kwa miezi mitano.

Kupitia ujumbe aliouandika kwenye mtandao wa kijamii Jumamosi jioni, Trump alisema washirika wa Marekani katika Mashariki ya Kati wamefikia msingi wa makubaliano ambayo yanaweza kuleta mwisho wa mzozo huo.

Kwa mujibu wa Trump, makubaliano hayo yanakusudia kuhakikisha Mlango wa Bahari wa Hormuz (Strait of Hormuz) unafunguliwa kikamilifu kwa usafiri wa kimataifa pamoja na kuondoa kile alichokiita tishio la mpango wa nyuklia wa Iran.

“Nimekubali kufuta mashambulizi yaliyokuwa yamepangwa kwa maslahi ya dunia na kwa mustakabali wa Iran yenye amani na maendeleo, mradi tu makubaliano yaweze kufikiwa kwa haraka,” alisema Trump.

Aidha, Trump alidai kuwa Israel imekubali kushirikiana na Marekani katika kuendeleza mazungumzo hayo ili kufikia makubaliano yatakayomaliza vita. Hata hivyo, hadi sasa Iran haijatoa tamko rasmi kuhusu kauli hiyo.

Tangazo hilo limekuja ikiwa ni siku moja tu baada ya Trump kuashiria kuwa Marekani ilikuwa ikikaribia kuanzisha tena mashambulizi makubwa dhidi ya Iran ili kuilazimisha kurejea kwenye mazungumzo.

Vita kati ya Marekani, Israel na Iran vilianza Februari 28, huku Marekani ikieleza kuwa operesheni hiyo ililenga kudhoofisha uwezo wa makombora wa Iran, kuzuia taifa hilo kutengeneza silaha za nyuklia na kukomesha uungaji mkono wake kwa makundi yenye silaha yanayoshirikiana nalo. Hata hivyo, malengo na mwelekeo wa operesheni hiyo yamekuwa yakibadilika mara kwa mara, huku makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa mwezi Juni yakivunjika ndani ya muda mfupi.

Wakati huo huo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imetoa tahadhari mpya kwa raia wake waliopo katika nchi za Mashariki ya Kati, ikiwataka kuwa waangalifu kutokana na uwezekano wa kufutwa kwa safari za ndege, kufungwa kwa baadhi ya anga na usumbufu mwingine wa usafiri. Tahadhari hizo zinahusu Bahrain, Israel, Iraq, Jordan, Kuwait, Lebanon, Oman, Qatar, Saudi Arabia na Falme za Kiarabu (UAE).

Leave a Comment