
Mwenyekiti wa Simba Sports Club, Murtaza Mangungu, amesema uteuzi wa baadhi ya wajumbe wapya wa uongozi wa klabu hiyo ulifanyika baada ya majadiliano kati yake na mfadhili wa klabu, Mohammed Dewji maarufu kama Mo Dewji.
Akizungumza leo Agosti 3, 2026 katika kipindi cha Crown, Mangungu alisema majina ya wajumbe waliochaguliwa yalipendekezwa kwa ushirikiano kati yake na Mohammed Dewji, ambapo Mo alichangia majina manne huku matatu yakitoka kwake.
“Hawa ambao wamechaguliwa jana ni mapendekezo ambayo mimi nilishauriana na Mohammed, tukapitisha. Mo amechangia majina manne, matatu yametoka kwangu,” alisema Mangungu.
Kuhusu suala la Amos Makalla, Mangungu amesema jina lake lilipendekezwa na Mohammed Dewji, huku akieleza kuwa uamuzi wa mwisho wa kukubali au kukataa nafasi hiyo utakuwa wa Makalla mwenyewe kwa kuwa bado hajapokea barua rasmi ya uteuzi.

“Mohammed ndiye aliyempendekeza. Kuhusu kumshauri au hakumshauri hilo si jukumu langu, lakini hata hivyo anayo haki ya kukubali au kukataa kwa sababu bado hajapewa barua ya uteuzi,” alisema.
Mangungu pia alisisitiza kuwa anathamini mchango wa Mohammed Dewji ndani ya Simba na kueleza kuwa uhusiano wao haujaanza kupitia klabu hiyo, bali ni wa muda mrefu zaidi ya miaka 20.
“Mimi ni mmoja kati ya watu wanaothamini mchango wa Mohammed Dewji na namheshimu kama anavyoniheshimu. Watu wanadhani nimemfahamu Mohammed kupitia Simba, mimi ni rafiki yangu zaidi ya miaka 20, pengine kabla ya hawa machawa wote,” alisema.

Katika mahojiano hayo, Mangungu pia alieleza kuwa alifanya jitihada za kuitisha mkutano wa dharura wa klabu kufuatia maelekezo aliyoyapokea kutoka Serikalini, lakini akasema alipendekeza kufanyika Agosti 2 na akaelezwa kuwa siku hiyo kulikuwa na shughuli ya marathon.
Ameendelea kusisitiza kuwa yeye ndiye Mwenyekiti wa Simba aliyechaguliwa na wanachama, huku akisema mabadiliko yoyote ndani ya klabu lazima yafanywe kwa kufuata taratibu za kisheria na maamuzi ya wanachama.