×

Vodacom Yazindua Kampeni ya “Zaidi ya Mtandao”, Yaahidi Kuwezesha Fursa Zaidi kwa Watanzania

Dar es Salaam, Agosti 4, 2026 – Vodacom Tanzania Plc imezindua rasmi kampeni mpya ya “Zaidi ya Mtandao” (More Than a Network), ikisisitiza dhamira yake ya kwenda mbali zaidi ya kutoa huduma za mawasiliano kwa kuwezesha fursa za maendeleo kwa watu binafsi, biashara na jamii nchini.

Kampeni hiyo inakuja wakati Vodacom ikiendelea kuongoza soko la mawasiliano Tanzania. Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) za robo ya mwaka iliyoishia Machi 2026, kampuni hiyo inaongoza kwa kuwa na asilimia 32.3 ya wateja wote wa huduma za mawasiliano nchini, sawa na zaidi ya wateja milioni 36.1.

Aidha, taarifa ya fedha ya Vodacom kwa robo ya mwaka iliyoishia Juni 2026 inaonyesha kampuni imeongeza uwekezaji wake hadi kufikia shilingi bilioni 123.2, karibu mara mbili ya kiwango kilichowekezwa katika kipindi kama hicho mwaka uliopita. Uwekezaji huo umeelekezwa katika kuboresha mtandao na mfumo wa M-Pesa, ukiwa sehemu ya mkakati wa kuharakisha ujumuishaji wa kidijitali na kuwafikia Watanzania wengi zaidi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Kitengo cha Biashara wa Vodacom Tanzania Plc, Brigita Shirima, alisema kampeni ya “Zaidi ya Mtandao” inalenga kuhakikisha teknolojia inazalisha matokeo yenye manufaa kwa jamii.

“Zaidi ya Mtandao ni ahadi yetu kwamba teknolojia na huduma tunazotoa lazima zilete matokeo chanya. Tunataka kumwezesha mwanafunzi kupata elimu ya kidijitali, kuiunganisha familia na kusaidia wajasiriamali kukuza biashara zao. Mtandao haupimwi kwa teknolojia pekee, bali kwa thamani na fursa unazozalisha kwa watu na jamii,” alisema Shirima.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Vodacom Business, Nguvu Kamando, alisema biashara za kisasa zinahitaji zaidi ya huduma za mawasiliano, zikihitaji suluhisho za kidijitali zitakazoongeza ushindani na ufanisi.

Alieleza kuwa Vodacom Business inaendelea kuwezesha kampuni, biashara ndogo na za kati pamoja na taasisi mbalimbali kupitia huduma za mawasiliano salama, teknolojia ya utunzaji wa kumbukumbu, Internet of Things (IoT) na majukwaa ya kidijitali yanayochochea ukuaji wa uchumi.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa M-Pesa Vodacom Tanzania Plc, Tulisindo Mlupilo, alisema M-Pesa inaendelea kuwa mhimili muhimu wa ujumuishaji wa kifedha nchini, ikiwa na zaidi ya watumiaji hai milioni 14.1 kila mwezi.

Alibainisha kuwa kupitia huduma kama M-KOBA, SONGESHA, M-WEKEZA na LIPA, mamilioni ya Watanzania wanaendelea kupata huduma za kifedha kwa urahisi, huku maboresho yanayoendelea ya mfumo wa M-Pesa yakitarajiwa kuongeza ufanisi na kupanua huduma zaidi.

Vodacom imesisitiza kuwa kampeni ya “Zaidi ya Mtandao” ni sehemu ya maono yake ya muda mrefu ya kutumia teknolojia kama nyenzo ya kuleta maendeleo, kukuza uchumi wa kidijitali na kuboresha maisha ya Watanzania kupitia huduma zenye thamani zaidi ya mawasiliano ya kawaida.

Leave a Comment