×

Salah Kutua Uturuki leo Kukamilisha Uhamisho Trabzonspor Baada ya Kuondoka Liverpool

ISTANBUL: Klabu ya Trabzonspor ya Uturuki imethibitisha kuwa ipo kwenye mazungumzo ya kumsajili nyota wa Misri, Mohamed Salah, huku ikitangaza kuwa mchezaji huyo anatarajiwa kuwasili Istanbul leo, Jumatano Agosti 5, 2026, kwa ajili ya mazungumzo ya mwisho kuhusu uhamisho wake.

Katika taarifa yake, Trabzonspor ilisema Salah atawasili Uwanja wa Ndege wa Ataturk jijini Istanbul kabla ya kuelekea Trabzon baadaye siku hiyo ikiwa sehemu ya mchakato wa kukamilisha usajili wake.

Salah, mwenye umri wa miaka 34, aliondoka Liverpool mwishoni mwa msimu uliopita baada ya kuitumikia klabu hiyo kwa miaka tisa yenye mafanikio makubwa. Akiwa Anfield, alishinda taji la UEFA Champions League, mataji mawili ya Ligi Kuu England na kuweka rekodi ya kufunga mabao 257 katika mechi 442, na kuwa mfungaji wa tatu bora katika historia ya Liverpool.

Nyota huyo pia amefunga mabao 193 katika Ligi Kuu England, yakiwemo 191 akiwa Liverpool, na kushika nafasi ya nne kwenye orodha ya wafungaji bora wa muda wote wa ligi hiyo.

Msimu uliopita haukuwa mzuri kwake wala kwa Liverpool, ambapo alifunga mabao saba pekee kwenye ligi, jambo lililochangia kuondoka kwake mwishoni mwa msimu.

Kwa upande wa timu ya taifa ya Misri, Salah ameifungia mabao 66 katika mechi 119 za kimataifa na anaendelea kutajwa miongoni mwa wachezaji bora zaidi kuwahi kutokea barani Afrika.

Trabzonspor ilimaliza nafasi ya tatu katika Ligi Kuu ya Uturuki msimu uliopita na kufuzu hatua ya mchujo ya Europa League, huku usajili wa Salah ukitarajiwa kuongeza nguvu katika kikosi hicho kuelekea msimu mpya.

Leave a Comment