×

Tanzania Yavutia Uwekezaji wa Huduma za Kifahari Viwanja vya Ndege

 Kampuni ya Plaza Premium Group (PPG), inayojihusisha na huduma za ukarimu katika viwanja vya ndege duniani, inatarajia kufungua ukumbi wake wa kwanza wa mapumziko kwa wasafiri (Plaza Premium Lounge) nchini Tanzania katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Terminal 3, mwishoni mwa Agosti mwaka huu.

Ufunguzi huo unatajwa kuwa sehemu ya mkakati wa kampuni wa kupanua uwekezaji wake nchini Tanzania huku ukiunga mkono juhudi za kuimarisha sekta za usafiri wa anga, utalii na biashara.

Katika maandalizi ya uzinduzi huo, PPG iliwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta za usafiri wa anga, utalii, fedha, biashara na taasisi za Serikali jijini Dar es Salaam kujadili fursa za ushirikiano katika kuboresha huduma kwa wasafiri na kuimarisha miundombinu ya ukarimu katika viwanja vya ndege.

Makamu wa Rais Mwandamizi wa Plaza Premium Group anayesimamia Kanda ya Ulaya, Mashariki ya Kati na Afrika (EMEA), Okan Kufeci, alisema Tanzania ni miongoni mwa masoko yenye ukuaji mkubwa katika sekta ya usafiri wa anga na utalii Afrika Mashariki.

Alisema ongezeko la uwekezaji katika miundombinu ya usafiri wa anga, kuongezeka kwa safari za kimataifa na ukuaji wa utalii vinaifanya Tanzania kuwa eneo lenye mazingira mazuri kwa uwekezaji katika huduma za kiwango cha kimataifa kwa wasafiri.

“Tunaona fursa kubwa ya kushirikiana na Serikali, mashirika ya ndege na wadau wengine kuboresha uzoefu wa wasafiri huku tukichangia maendeleo ya sekta ya usafiri wa anga nchini Tanzania,” alisema Kufeci.

Kwa mujibu wa kampuni hiyo, Plaza Premium Lounge itatoa huduma mbalimbali kwa wasafiri kabla ya safari zao, zikiwemo chakula na vinywaji vya viwango vya kimataifa, maeneo ya kisasa ya kupumzikia, mabafu, chumba cha ibada, huduma za biashara na huduma nyingine binafsi zinazolenga kuongeza faraja kwa wasafiri.

PPG inaeleza kuwa huduma hizo zitachanganya viwango vya kimataifa vya kampuni hiyo na ukarimu wa Kitanzania ili kuwapatia wasafiri uzoefu bora wanapotumia JNIA.

Uwekezaji huo pia unatarajiwa kuunga mkono azma ya Tanzania ya kuifanya JNIA kuwa kitovu muhimu cha usafiri wa anga, biashara na utalii katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Plaza Premium Group inafanya shughuli zake katika zaidi ya viwanja vya ndege 600 vilivyopo katika nchi 150 duniani na kuhudumia zaidi ya wasafiri milioni 30 kila mwaka. Kampuni hiyo pia imejishindia zaidi ya tuzo 180 za kimataifa kutokana na ubora wa huduma zake, ikiwemo tuzo ya World’s Best Independent Airport Lounge iliyotolewa na Skytrax kwa miaka tisa mfululizo kuanzia mwaka 2016 hadi 2025.

Leave a Comment