×

Yanga Yazindua Jezi Mpya za Msimu wa 2026/27, Wanayanga Wavamia Jangwani – Video

Klabu ya Young Africans SC (Yanga) imezindua rasmi jezi zake mpya zitakazotumika katika msimu wa mashindano wa 2026/27, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuanza kwa msimu mpya wa soka.

Jezi hizo mpya zenye miundo mitatu tofauti kwa ajili ya mechi za nyumbani, ugenini na jezi mbadala, zimeendelea kubeba rangi na utambulisho wa klabu hiyo kupitia mchanganyiko wa kijani, njano na nyeusi.

Baada ya kutambulishwa rasmi, jezi hizo zimepokelewa kwa hamasa kubwa na mashabiki wa Yanga ambao wamejitokeza kwa wingi katika Makao Makuu ya klabu hiyo, Jangwani jijini Dar es Salaam, wakitaka kupata nakala zao mpya.


Uzinduzi huo umefanyika kupitia kurasa rasmi za mitandao ya kijamii za klabu hiyo kuanzia saa tano asubuhi leo, Agosti 6, 2026, huku mashabiki wakiendelea kuonyesha shauku kubwa kuelekea msimu mpya.

Katika hafla hiyo, baadhi ya wachezaji wa kikosi cha kwanza cha Yanga walionekana wakiwa wamevalia jezi hizo mpya, ishara ya kuanza rasmi kwa safari ya msimu wa 2026/27 ambao klabu hiyo inalenga kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kufanya vizuri zaidi katika mashindano ya kimataifa ya CAF.

Mbali na uzinduzi wa jezi, shughuli nyingine za kijamii zinaendelea kuelekea kilele cha Tamasha la Yanga Day litakalofanyika Agosti 9, 2026 katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam. Wanachama na mashabiki wa klabu hiyo wameendelea kujitokeza kwa wingi katika zoezi la uchangiaji damu linaloendelea sambamba na maandalizi ya tukio hilo kubwa.

Jezi mpya za Yanga zinatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya utambulisho wa klabu hiyo katika msimu ujao, huku mashabiki wakitarajia kuona mafanikio zaidi ndani na nje ya Tanzania.

Leave a Comment