×

Matthew McConaughey na Mkewe Wakutana na Papa Leo XIV Vatican

Muigizaji maarufu wa Hollywood Matthew McConaughey akisalimiana na Pope Leo XIV katika Kanisa la Mtakatifu Petro (St. Peter’s Basilica), Vatican City, Agosti 5, 2026.

Muigizaji maarufu wa Hollywood Matthew McConaughey na mkewe Camila Alves McConaughey wamekutana na Pope Leo XIV katika Kanisa la Mtakatifu Petro (St. Peter’s Basilica), Vatican City, wakati wa hadhara ya kila wiki ya Papa iliyofanyika Agosti 5, 2026.

Katika picha zilizosambaa, McConaughey alionekana akisalimiana kwa mkono na Papa Leo XIV huku Camila akitabasamu pembeni. Ziara hiyo imevutia hisia za wengi, hasa ikizingatiwa kuwa wanandoa hao wamekuwa wakitumia muda mwingi nchini Italia katika miezi ya hivi karibuni.

McConaughey, mwenye umri wa miaka 56, yupo nchini Italia akirekodi filamu mpya ya Netflix inayoitwa Positano, ambapo anaigiza pamoja na Zoe Saldaña. Filamu hiyo inamhusu mwizi wa vito anayekubali kumsaidia mwanamke mwenye siri kutekeleza wizi mkubwa.

Muigizaji maarufu wa Hollywood Matthew McConaughey akiwa na mkewe Camila Alves

Kwa upande wake, Camila Alves amekuwa akishiriki picha na video mbalimbali kutoka matukio ya mitindo nchini Italia, ikiwemo maonesho ya kifahari ya Dolce & Gabbana Alta Moda yaliyofanyika Sicily.

McConaughey amekuwa wazi kwa miaka mingi kuhusu imani yake ya Kikristo. Mwaka 2025 alichapisha kitabu cha mashairi na tafakari kiitwacho Poems & Prayers, ambapo alieleza jinsi imani ilivyomsaidia katika nyakati za mafanikio na changamoto. Pia alikiri kuwa aliwahi kupitia kipindi cha kutokuwa na uhakika wa imani kabla ya kurejea kwa Mungu.

Papa Leo XIV, aliyechaguliwa kuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki mwezi Mei 2025, ndiye Papa wa kwanza kutoka Marekani katika historia ya Kanisa Katoliki.

Leave a Comment