Rais Samia Azindua BRT Awamu ya Pili, Safari Gerezani–Mbagala Yaanza (Picha +Video)
Global Publishers August 7, 2026 1,146 views 0 Comments
SHARE THIS:
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan akitumia kadi ya kidigitali kuingia katika Kituo cha abiria cha mabasi yaendayo haraka cha Water front, jijini Dar es Salaam, kabla ya kuelekea Mtoni kwa Aziz Ally kwa ajili ya kufungua Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka, Awamu ya Pili (BRT II) unaohusisha Barabara ya Kilwa, Chang’ombe, Sokoine na Kawawa, Jijini Dar es Salaam, tarehe 07 Agosti, 2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Agosti 7, 2026, amezindua rasmi Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka BRT Awamu ya Pili (BRT II) katika eneo la Mtoni kwa Aziz Ali, jijini Dar es Salaam.
Uzinduzi huo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuboresha huduma za usafiri wa umma, kupunguza msongamano wa magari na kurahisisha usafiri kwa wakazi wa Dar es Salaam.
Rais Dkt. Samia akivuta kitambaa pamoja na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Sidi Ould Tah kuashiria ufunguzi wa Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka, Awamu ya Pili (BRT II) unaohusisha Barabara ya Kilwa, Chang’ombe, Sokoine na Kawawa, Jijini Dar es Salaam, tarehe 07 Agosti, 2026.
Awamu ya pili ya BRT inahusisha njia yenye urefu wa takribani kilomita 20.3, kutoka Gerezani hadi Mbagala kupitia Barabara ya Kilwa. Mradi huo umeunganishwa na Awamu ya Kwanza ya BRT, hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa mtandao wa usafiri wa umma jijini.
Tofauti nyingine muhimu katika awamu hii ni matumizi ya mabasi yanayotumia gesi asilia iliyobanwa (CNG). Teknolojia hiyo inalenga kupunguza uchafuzi wa mazingira, kupunguza gharama za uendeshaji pamoja na kuongeza ufanisi wa huduma.
Mradi huo unatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kuboresha usafiri kwa wakazi wanaotumia korido ya Kilwa, hususan katika maeneo ya Mbagala na vitongoji vinavyounganishwa na njia hiyo.
Rais Samia akiwa ndani ya basi liendalo haraka wakati akielekea Mtoni kwa Aziz Ally, kufungua Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka, Awamu ya Pili (BRT II) unaohusisha Barabara ya Kilwa, Chang’ombe, Sokoine na Kawawa, Jijini Dar es Salaam, tarehe 07 Agosti, 2026.Rais Samia akikata utepe pamoja na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Sidi Ould Tah kuashiria ufunguzi wa Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka, Awamu ya Pili (BRT II) .