×

UNICEF: Watoto 300 Wameuawa Gaza Ndani ya Siku 300, Maelfu ya Wapalestina Wahamishwa

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limesema kuwa angalau watoto 300 wameuawa katika Ukanda wa Gaza ndani ya siku 300 zilizopita, wastani wa mtoto mmoja kwa siku, huku mashambulizi makali ya kijeshi yakiendelea kuathiri raia.

UNICEF iliongeza kuwa mamia ya watoto wengine wameripotiwa kujeruhiwa katika kipindi hicho.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA), watoto wa Gaza wanaendelea kuishi katika mazingira magumu yanayojumuisha makazi yenye msongamano mkubwa, pamoja na uhaba wa maji salama na huduma za afya.

Katika Ukingo wa Magharibi (West Bank), OCHA imesema mashambulizi ya walowezi wa Israel na operesheni za kijeshi za Israel zinaendelea kuathiri makazi na maisha ya Wapalestina.

Shirika hilo liliripoti kuwa walowezi wa Israel walichoma moto nyumba katika kijiji cha Tuba, eneo la Masafer Yatta, karibu na Hebron, na kusababisha familia tatu, zikiwemo watoto 14, kukimbia makazi yao na kutafuta hifadhi kwa ndugu na majirani.

Aidha, watu kadhaa walijeruhiwa, wakiwemo watoto wawili, huku mfumo wa nishati ya jua, tani 10 za chakula cha mifugo na mali nyingine zikiharibiwa.

OCHA ilisema kuwa kati ya Januari na mwisho wa Julai mwaka huu, ilirekodi matukio zaidi ya 1,380 yaliyohusisha walowezi wa Israel na kusababisha majeruhi, uharibifu wa mali au yote mawili. Pia zaidi ya Wapalestina 2,300 walilazimika kuhama makazi yao kutokana na mashambulizi hayo na vikwazo vya upatikanaji wa maeneo mbalimbali.

Shirika hilo limetoa wito wa kulindwa kwa Wapalestina katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na kuwawajibisha wote wanaohusika na mashambulizi dhidi ya raia.

Wakati huo huo, katika eneo la Qalandia lililoko Mkoa wa Jerusalem, maelfu ya Wapalestina waliendelea kuzuiliwa kwa siku ya pili mfululizo kufuatia operesheni kubwa ya jeshi la Israel. OCHA ilisema wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu hawakuweza kuingia eneo hilo kwa usalama, hali iliyozua wasiwasi kuhusu upatikanaji wa huduma za dharura na huduma nyingine muhimu kwa wakazi.

Leave a Comment