
07.08.2026 | Dodoma. Wakulima wa Kanda ya Kati wanaotumia huduma za kifedha za Mixx by Yas kupitia vyama vya ushirika wameendelea kunufaika na malipo ya kidijitali pamoja na zawadi mbalimbali, hatua inayosaidia kuongeza usalama wa fedha, kuharakisha malipo na kuhamasisha uzalishaji wa mazao.
Akizungumza katika hafla ya Vuna na Mixx iliyofanyika wakati wa Maonesho ya Nanenane jijini Dodoma, Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, alisema ushirikiano kati ya Tume hiyo na Mixx by Yas umeleta mabadiliko katika mfumo wa malipo kwa wakulima wanaouza mazao kupitia mfumo wa stakabadhi za ghala.
Alisema matumizi ya malipo ya kidijitali yamesaidia kupunguza changamoto zilizokuwa zikihusishwa na matumizi ya fedha taslimu, ikiwemo ucheleweshaji wa malipo na hatari ya kupotea kwa fedha, huku wakulima wakipokea fedha zao kwa usalama na kwa wakati.
“Malipo yanapowafikia wakulima kwa wakati yanawapa motisha ya kuongeza uzalishaji. Tumeona mabadiliko makubwa katika mfumo wa ushirika na ongezeko la mazao kutokana na kuimarika kwa huduma hizi,” alisema Dkt. Ndiege.
Dkt. Ndiege aliwataka wakulima wanaonufaika na mfumo huo kuwa mabalozi wa matumizi ya huduma za kifedha kidijitali kwa kuwahamasisha wakulima wengine kujiunga na kutumia huduma hizo.
Aidha, aliwapongeza maafisa ushirika pamoja na viongozi wa vyama vya ushirika vya msingi (AMCOS) kwa kuendelea kutoa elimu inayowawezesha wakulima kutumia huduma hizo kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Meneja wa Biashara wa Mixx Kanda ya Kati, Bw. Charles Gasper, alisema kampuni hiyo imeendelea kushirikiana na Serikali pamoja na vyama vya ushirika kuhakikisha wakulima wanapata huduma za kifedha zilizo salama, rahisi na za haraka.
Gasper alisema katika hafla hiyo, Mixx iliwatunuku zawadi wakulima zaidi ya 25 kutoka Kanda ya Kati waliotumia huduma zake kupitia vyama vya ushirika.
Zawadi hizo zilijumuisha pikipiki, maguta na baiskeli, ikiwa ni sehemu ya kutambua na kuhamasisha matumizi ya huduma za kifedha za kidijitali miongoni mwa wakulima.
“Tunaamini tukimwezesha mkulima, tunachangia ukuaji wa familia yake, jamii na uchumi wa taifa. Hivyo tutaendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya kilimo kuhakikisha wakulima wengi zaidi wananufaika na huduma za Mixx,” alisema Gasper.
Hafla hiyo imeongeza msukumo wa matumizi ya huduma za kifedha kidijitali katika sekta ya kilimo, huku wakulima wakihimizwa kutumia teknolojia kurahisisha upokeaji wa malipo na kuongeza ufanisi katika shughuli zao.