
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema Tamasha la Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, lina msingi wa kuhifadhi na kuendeleza utamaduni, mila na desturi za watu wa Zanzibar.
Aidha, chama hicho kimesema tamasha hilo linalenga kuanzisha, kuendeleza na kuibua miradi ya kiuchumi na kimaendeleo katika jamii.
Hayo yameelezwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, wakati akizungumza na waandishi wa habari waliofika katika ofisi yake Kisiwandui, Zanzibar.
Mbeto amesema Tamasha la Kizimkazi halina sura ya kisiasa, bali limejielekeza katika kuonesha ustaarabu, mila, utamaduni, silka, akhlaq, michezo na shughuli mbalimbali za wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja.
Amesema kila jamii hutofautiana katika tabia, shughuli za uzalishaji mali, masuala ya kiuchumi na kijamii, ikiwemo ngoma, unyago, jando, harusi pamoja na mikusanyiko ya jadi na asili za watu wake.
“Kuna mikusanyiko isiyopishana sana kwa mila, utamaduni, ustaarabu, ngoma za asili, lahaja na matamshi ya lugha ya Kiswahili baina ya mkoa hadi kisiwa kimoja na kingine,” amesema Mbeto.
Aidha, amesema tamasha hilo huonesha aina mbalimbali za mapishi ya Mkoa wa Kusini Unguja, shughuli za uzalishaji mali, sanaa, ufundi stadi, kazi za mikono pamoja na maeneo ya kihistoria.
Mbeto amesema pia tamasha hilo linatoa nafasi ya kuwasilisha hadithi na simulizi za kihistoria zinazohusu wenyeji pamoja na wageni na wahamiaji wa kale waliofika na kuishi Kizimkazi.
Amesema simulizi hizo zinatofautiana na zile zinazopatikana katika maeneo mengine ya Zanzibar, ikiwemo Unguja, Tumbatu na Pemba.
Katibu huyo amesema hata katika mapokeo ya harakati za kisiasa kuna mitazamo na ushiriki wa jamii, kwa kuwa siasa haiwezi kutenganishwa na maisha ya jamii, juhudi na harakati za watu katika kujikomboa na kuleta maendeleo.
“Tamasha la Kizimkazi la kila mwaka huwaunganisha wanajamii na kuwaweka pamoja. Mikusanyiko hiyo huhimiza umoja, ushirikiano, upendo na udugu,” amesisitiza.
Mbeto pia ameeleza kuwa hatua ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutembea mitaani ndani ya Hifadhi ya Mji Mkongwe, kusalimiana na wenyeji pamoja na watalii, ni sehemu ya kuhimiza umoja na upendo.
“Dunia ya leo inahitaji maelewano, si migawanyiko,” amesema Mbeto.
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar