
Zaidi ya kampuni 10 za biashara ya masoko zimeanza kutumia huduma mpya ya kampuni ya Trump Media inayowapa fursa ya kupata kwa haraka machapisho yanayowekwa kwenye mtandao wa kijamii wa Truth Social, huku baadhi yao zikilipa hadi dola 100,000 za Marekani, sawa na takribani TSh milioni 260, kwa mwezi.
Huduma hiyo inayojulikana kama Truth API ilianza kutolewa mwanzoni mwa Agosti, ikiwa na lengo la kuwapa wafanyabiashara wa masoko taarifa za mapema kutoka kwa akaunti zenye ushawishi mkubwa katika Truth Social.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa muda wa Trump Media, Kevin McGurn, wateja wa mwanzo wa huduma hiyo ni zaidi kampuni zinazofanya biashara za masoko kwa kasi kubwa, ambazo zinatozwa kati ya dola 60,000 na dola 100,000 kwa mwezi, sawa na takribani TSh milioni 156 hadi TSh milioni 260.
Huduma hiyo imezua mjadala kutokana na uwezekano wa wafanyabiashara kuitumia taarifa hizo kufanya maamuzi ya haraka katika masoko ya hisa na mali nyingine kabla ya taarifa hizo kuwafikia watumiaji wengine.
Truth Social ni jukwaa ambalo Rais wa Marekani, Donald Trump, hutumia mara kwa mara kutoa kauli na matangazo ambayo wakati mwingine yanaweza kuathiri mwenendo wa masoko.
Trump Media ilitangaza mwezi Julai mpango wa kuwapa taasisi za kifedha na wawekezaji wakubwa fursa ya kupata machapisho hayo kwa kasi zaidi.
Mpango huo umeibua maswali ya kimaadili na kisheria, hasa kutokana na ukweli kwamba familia ya Trump bado ina umiliki mkubwa katika kampuni hiyo. Hoja kubwa ni iwapo kampuni hiyo inapaswa kunufaika kifedha kutokana na taarifa zinazotolewa hadharani na Rais.
Trump Media imesema Truth API inatarajiwa kuwa chanzo kipya cha mapato na inaweza kuwa sehemu muhimu ya mkakati wake wa biashara kwa muda mrefu.
Mbali na kampuni za biashara ya masoko, kampuni hiyo pia imeanza kutafuta fursa za kushirikiana na kampuni za teknolojia, mashirika ya habari na sekta ya masoko ya ubashiri.
Wakati huo huo, Trump Media imeripoti mapato ya dola milioni 1.7, sawa na takribani TSh bilioni 4.4, katika kipindi cha Aprili hadi Juni, ikiwa ni ongezeko la asilimia 89 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.
Pamoja na ongezeko hilo la mapato, kampuni iliripoti hasara ya dola milioni 238, sawa na takribani TSh bilioni 619, ambayo ni zaidi ya mara 10 ya hasara iliyopata katika kipindi kama hicho mwaka uliopita.
Trump Media imesema sehemu kubwa ya changamoto zake za kifedha imetokana na shughuli zake zinazohusiana na sarafu za kidijitali, huku kampuni ikiendelea kupanua uwekezaji wake katika maeneo mapya, yakiwemo nishati safi.
Mchambuzi Markus Thielen wa 10x Research amesema kampuni hiyo kwa sasa inaonekana kuwa imejikita zaidi katika biashara ya sarafu za kidijitali kuliko shughuli zake za awali za habari na mitandao ya kijamii.
Hata hivyo, Trump Media inasema inaendelea kutafuta vyanzo vipya vya mapato kupitia Truth Social na shughuli nyingine za biashara.
Mapema Agosti, kampuni hiyo pia ilisitisha mpango wa kushirikiana na Crypto.com kuanzisha huduma za masoko ya utabiri kwenye Truth Social.