
Washington, D.C. — Rais wa Marekani, Donald Trump, ametangaza kwamba Karoline Leavitt ataondoka katika nafasi yake ya Katibu wa Habari wa White House mwishoni mwa Agosti 2026, huku akisema uamuzi huo umetokana na nia yake ya kutumia muda zaidi na watoto wake wadogo na familia.
Trump alitoa taarifa hiyo Jumatano, Agosti 12, akimtaja Leavitt kuwa mmoja wa wasaidizi wake anaowaamini zaidi na kumsifu kwa kazi kubwa aliyofanya katika utawala wake.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Leavitt hataondoka kabisa katika siasa za Trump. Baada ya kuondoka White House, ataendelea kuwa mshauri wa nje wa Trump na kuwa na ushawishi ndani ya Chama cha Republican, hasa wakati chama hicho kikijiandaa kwa uchaguzi wa katikati ya muhula, maarufu kama midterm elections.
Trump amemsifu Leavitt kwa uongozi wake katika White House, akisema amefanya kazi ya kipekee katika kutetea misimamo ya utawala wake kuhusu haki, uhuru na masuala mengine ya kisiasa.
Leavitt, mwenye umri wa miaka 28, aliteuliwa kuwa Katibu wa Habari wa White House mwaka 2025 na kuwa mtu mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kushika nafasi hiyo. Kabla ya hapo, aliwahi kufanya kazi katika utawala wa kwanza wa Trump na pia alikuwa sehemu ya kampeni yake ya uchaguzi wa mwaka 2024.

Uamuzi wake unakuja muda mfupi baada ya kurejea kazini kufuatia likizo ya uzazi. Leavitt alikuwa amesitisha majukumu yake ya mbele tangu Aprili kabla ya kujifungua mtoto wake wa pili, binti aitwaye Viviana, mwezi Mei. Alirejea rasmi kwenye nafasi yake na kufanya mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari baada ya likizo hiyo Julai 16.
Trump amesema anaelewa na kuheshimu uamuzi wa Leavitt, akisisitiza kuwa ataendelea kuwa mtu muhimu katika timu yake hata baada ya kuondoka White House.
Kwa sasa, jina la atakayechukua nafasi ya Leavitt kama Katibu wa Habari wa White House halijatangazwa rasmi. Kuondoka kwake kunatarajiwa kuleta mabadiliko katika timu ya mawasiliano ya utawala wa Trump wakati Marekani ikielekea kwenye uchaguzi wa midterm wa 2026.