×

Mwamnyeto na Mngqithi Watoa Kauli Ya Kibabe Kukiwasha Dhid Namungo Kesho

Kocha Mkuu wa Yanga SC, Manqoba Mngqithi

Beki wa Yanga SC, Bakari Mwamnyeto, amesema morali ndani ya kikosi hicho ipo juu kuelekea mchezo wao wa kwanza wa ligi dhidi ya Namungo FC, huku akisisitiza kuwa wamejiandaa kuhakikisha wanaondoka na alama tatu.

Yanga inatarajiwa kushuka dimbani Jumamosi, Agosti 15, 2026, kukutana na Namungo FC katika Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa, Lindi, katika mchezo unaotarajiwa kuanza saa 3:00 usiku.

Mwamnyeto amesema wanatambua kuwa Namungo ni timu yenye wachezaji wazuri pamoja na benchi la ufundi lenye uwezo, hivyo hawatarajii kupata ushindi kwa urahisi.

Sisi pia ni wazuri na tuna kikosi imara zaidi. Kwa hiyo, atakayocheza vizuri ndiye atakayeshinda. Mimi naamini tutaondoka na alama zetu tatu kesho,”amesema Mwamnyeto.

Beki wa Yanga SC, Bakari Mwamnyeto

Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Yanga SC, Manqoba Mngqithi, amewapongeza mashabiki wa klabu hiyo waliofika Lindi na kuwataka waendelee kuwa sehemu muhimu ya safari ya timu hiyo.

Mngqithi amesema uwepo wa mashabiki uwanjani unawapa wachezaji morali na nguvu zaidi wanapokuwa kwenye uwanja wa mapambano.

“Nimefurahi sana kuwaona mashabiki wetu hapa Lindi. Ninaamini kuwa kila siku watakuwa wachezaji wetu wa 12 uwanjani. Kwa kweli watatusaidia sana kucheza kwa morali na nguvu tunapokuwa uwanjani. Natamani kuwaona tena kesho kwenye mechi yetu dhidi ya Namungo,” amesema Mngqithi.

Kocha huyo amesema licha ya Yanga kutokuwa na muda mrefu wa kujiandaa mahsusi kwa mchezo huo, anaamini maandalizi yaliyofanyika tangu mchezo wa Derby yamewapa msingi mzuri wa kukabiliana na Namungo.

Hatujapata muda mrefu wa kujiandaa dhidi ya Namungo, lakini kwa namna tulivyojipanga tangu mchezo wa Derby naamini tutakuwa kwenye mfumo wetu ule ule na ninaamini tutapata matokeo mazuri,”** amesema.

Mchezo huo utakuwa muhimu kwa Yanga katika kuanza rasmi kampeni ya kutetea ubingwa wa NBC Premier League, huku Namungo ikiwa na dhamira ya kuanza msimu kwa matokeo mazuri mbele ya mashabiki wake.

Macho ya mashabiki sasa yanaelekezwa Lindi, wakisubiri kuona kama Yanga itatimiza ahadi ya Mwamnyeto ya kuondoka na alama tatu au Namungo itaweka kikwazo katika mwanzo wa safari ya mabingwa hao watetezi.

Stori na Na Haika Urio | GPL

Leave a Comment