
Dar es Salaam — Mkurugenzi wa JATU PLC, Peter Gasaya, pamoja na wenzake wanne wameachiwa na kurejea uraiani baada ya kukaa mahabusu kwa takribani miaka mitatu na miezi minane wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.
Gasaya na wenzake Nicholaus Fuime, Esther Kiya, Mariam Mrutu pamoja na JATU PLC, wamefikia makubaliano na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kupitia utaratibu wa plea bargaining, unaowezesha pande mbili kufikia makubaliano ya kisheria kuhusu namna ya kumaliza shauri.
Baada ya makubaliano hayo, watuhumiwa hao walirejea uraiani jana, Agosti 14, 2026.
Katika hatua nyingine, mali za JATU PLC zilizokuwa zikishikiliwa wakati wa kesi hiyo zimeelezwa kurejeshwa kwa Jatu Saccos, ambaye alikuwa mlalamikaji katika shauri hilo.
Gasaya na wenzake walifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu tarehe 29 Desemba 2022. Tangu wakati huo walikaa mahabusu huku kesi yao ikiendelea katika hatua mbalimbali za kisheria.
Hata hivyo, mwisho wa kesi hiyo hauwahusu wote waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka. Habiba Magero, Mariam Kusa-ja na Lucy Izengo bado wataendelea na kesi yao, ambayo imepangwa kusikilizwa tena Agosti 20, 2026.
Hatua hiyo imehitimisha kipindi kirefu cha kukaa mahabusu kwa Gasaya na wenzake wanne, huku mchakato wa kisheria ukiendelea kwa washtakiwa wengine watatu.