×

Trump Aomba Mahakama Kuruhusu Ujenzi wa Ukumbi wa Ikulu Kuendelea

WASHINGTON — Rais wa Marekani, Donald Trump, kupitia utawala wake, umeomba Mahakama ya Juu ya Marekani iruhusu kuendelea kwa ujenzi wa ukumbi mkubwa wa White House wenye thamani wa dola milioni 400 sawa na TSh trilioni 1.06.

Maombi hayo ya dharura yaliwasilishwa Ijumaa, Agosti 14, 2026 huku serikali ikipinga uamuzi wa mahakama za chini uliosimamisha sehemu ya ujenzi unaofanyika juu ya ardhi. Serikali inataka Mahakama ya Juu isimamishe kwa muda amri hiyo wakati mchakato wa kisheria ukiendelea.

Utawala wa Trump unasema mradi huo una umuhimu mkubwa kwa usalama wa taifa, ukidai kuwa jengo hilo halitakuwa ukumbi wa sherehe pekee bali pia litakuwa sehemu ya miundombinu ya usalama wa White House.

Kwa mujibu wa nyaraka zilizowasilishwa Mahakama ya Juu, mradi huo unahusisha maeneo yenye ulinzi mkubwa, ikiwemo miundombinu ya kukabiliana na mashambulizi, makazi ya dharura na vifaa vya kijeshi na kitabibu. Serikali pia inasema ukumbi huo unafadhiliwa kwa TSh trilioni 1.06 kutoka kwa wafadhili binafsi, bila kutumia fedha za walipa kodi.

Mvutano huo ulianza baada ya National Trust for Historic Preservation kufungua kesi kupinga mradi huo, ikidai kuwa ukubwa wake unaweza kuathiri thamani ya kihistoria na usanifu wa White House.

Mahakama ya chini ilizuia sehemu kubwa ya ujenzi, huku ikiruhusu kazi za chini ya ardhi zinazohusiana na usalama kuendelea. Serikali sasa inadai kuwa kusimamisha ujenzi huo kunaweza kuhatarisha usalama wa Rais, familia yake, wafanyakazi na viongozi wengine wanaotembelea White House.

Kwa upande mwingine, wapinzani wa mradi huo wanasisitiza kuwa hoja za usalama wa taifa hazipaswi kutumika kama sababu ya kupuuza sheria na taratibu zinazolinda maeneo ya kihistoria.

Serikali imeeleza kuwa mradi huo umefikia takribani asilimia 65 ya utekelezaji, hivyo inataka ujenzi uendelee badala ya kusimamishwa katika hatua hii.

Leave a Comment