×

Bilionea wa Majengo Afungwa Maisha Jela, Mali Zake Zataifishwa

Mwanzilishi wa kampuni kubwa ya ujenzi wa majengo nchini China, Evergrande, Hui Ka Yan, amehukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya makosa ya kifedha, hatua inayoashiria anguko la kampuni hiyo lililotikisa soko la nyumba nchini China.

Hui, ambaye pia anafahamika kwa jina la Xu Jiayin, alikiri makosa kadhaa mwezi Aprili, yakiwemo ubadhirifu wa mali na rushwa katika kampuni. Mahakama ya Kati ya Shenzhen pia iliamuru mali zake binafsi kuchukuliwa.

Aidha, kampuni zake za zamani zimepigwa faini ya yuan bilioni 15.82 sawa na TSh trilioni 6.19.

Faini hizo zinahusiana na makosa mbalimbali, ikiwemo kughushi taarifa za kampuni na kuficha madeni.

Mahakama ilisema mwenendo wa Hui na kampuni zake uliathiri kwa kiasi kikubwa soko la mali isiyohamishika nchini China na kusababisha hasara kubwa za kiuchumi.

Hui si mtendaji pekee wa Evergrande aliyehukumiwa. Watendaji wengine wa kampuni hiyo, akiwemo wanawe Xu Zhijian na Xu Tenghe, wamepewa vifungo vya kati ya miezi 22 na miaka 18, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali nchini China.

Kutoka utajiri hadi gerezani

Anguko la Hui ni la kushangaza kutokana na jinsi alivyowahi kuwa na nguvu kubwa katika sekta ya biashara nchini China. Alikulia katika mazingira ya kawaida vijijini na kulelewa na bibi yake kabla ya kuingia katika biashara ya ujenzi wa majengo.

Mwaka 1996, alianzisha Evergrande na kuanza kulipanua kwa kasi. Kampuni hiyo ilitumia mikopo mikubwa kufadhili miradi yake, na hatimaye ikawa moja ya makampuni makubwa zaidi ya ujenzi wa nyumba nchini China.

Leave a Comment