×

Simba Yarudi Meja Isamuhyo, Yafichua Ratiba Yake Kimataifa

Klabu ya Simba leo Agosti 24, 2026  imetangaza kurejea kutumia Uwanja wa Meja Isamuhyo kama uwanja wake wa nyumbani katika mechi za Ligi Kuu ya NBC, baada ya awali kutangaza kutumia Uwanja wa Uhuru.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, Semaji wa Simba, Ahmed Ally, amesema uamuzi huo umetokana na mafanikio ambayo timu hiyo ilipata msimu uliopita ilipotumia Meja Isamuhyo, akisema uwanja huo umekuwa sehemu salama kwa Simba.

“Msimu uliopita ambao tulicheza kwenye Uwanja wa Meja Isamuhyo hatukupoteza mchezo hata mmoja, ni sehemu salama kwelikweli kwa upande wetu,” amesema Ahmed Ally.

Amesema Simba itaanza kutumia uwanja huo kwenye mchezo dhidi ya Coastal Union, unaotarajiwa kuchezwa Agosti 27, 2026.

Katika mchezo huo, kiingilio kimewekwa Sh5,000 kwa jukwaa la Mzunguko na Sh10,000 kwa VIP A. Pia Simba imewataka mashabiki wake kujiandaa kutumia mfumo mpya wa ununuzi wa tiketi kwa njia ya simu.

Ahmed amesema mfumo huo unalenga kuwawezesha mashabiki kununua tiketi wakiwa walipo bila kulazimika kwenda vituoni kupanga foleni.

Mbali na Ligi Kuu, Simba imeeleza mipango yake katika mashindano ya kimataifa, ambapo itaanza hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mighty Wanderers ya Malawi.

Mchezo wa kwanza utachezwa Septemba 6, 2026 nchini Malawi, huku mechi ya marudiano ikipangwa Septemba 13, 2026 jijini Dar es Salaam. Simba imesema uwanja utakaotumika katika mchezo wa marudiano utatangazwa baadaye.

Kikosi cha Simba kinatarajiwa kuondoka nchini Septemba 4 kuelekea Malawi, ambapo kitafanya mazoezi siku hiyo na Septemba 5 kabla ya kushuka dimbani Septemba 6.

Ahmed Ally amesema Simba imefanya tathmini ya kutosha baada ya kushindwa kufuzu hatua ya robo fainali msimu uliopita, huku usajili wa wachezaji wenye uzoefu ukitajwa kuwa sehemu ya mkakati wa kurejea kwenye ushindani mkubwa Afrika.

“Ni imani yetu mwaka huu tutavuka hatua ya makundi na kwenda robo fainali. Malengo yetu makubwa ya msimu huu kimataifa ni kucheza hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika,” amesema.

Simba pia imeandaa safari maalum ya basi kwa mashabiki wake watakaotaka kwenda Malawi kuishangilia timu dhidi ya Mighty Wanderers.

Safari hiyo itaanza Septemba 3, 2026 saa 1 usiku kutoka Ubungo, Dar es Salaam, kuelekea Lilongwe, Malawi.

Klabu hiyo imesema inalenga kuwa na angalau mabasi matatu ya mashabiki, huku wanaotaka kusafiri wakitakiwa kuwa na hati ya kusafiria.

Kwa mujibu wa Ahmed Ally, safari hiyo inalenga kuongeza nguvu ya mashabiki kwa timu na kuvunja rekodi ya idadi ya Wanasimba watakaosafiri kwenda kuishangilia timu yao nje ya nchi.

Leave a Comment