×

Tume ya Jaji Lila Yaanza Kazi, Wahusika wa Ghasia za Uchaguzi Kuchunguzwa

Mwenyekiti wa Tume ya Kuchunguza Wahusika, Ghasia na Ukiukwaji wa Sheria, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Shaban Ally Lila.

Dar es Salaam, Agosti 24, 2026 — Tume ya Kuchunguza Wahusika, Ghasia na Ukiukwaji wa Sheria Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 imeanza rasmi kazi, huku Mwenyekiti wake, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Shaban Ally Lila, akieleza kuwa lengo kuu ni kubaini wahusika wa ghasia hizo na namna walivyoshiriki.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Jaji Lila amesema Tume hiyo imepewa jukumu la kuchunguza matukio ya ghasia, uvunjifu wa amani na madhara yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi huo.

Amesema Tume itachunguza pia chanzo cha ghasia hizo pamoja na ukiukwaji wa sheria uliojitokeza, ikiwemo kubaini watu waliohusika katika kupanga, kufadhili, kuratibu na kutekeleza matukio hayo.

Kwa mujibu wa Jaji Lila, Tume hiyo ina jukumu tofauti na Tume iliyokuwa chini ya Jaji Mstaafu Othman Chande, ambayo ilichunguza zaidi matukio ya ghasia na madhara yaliyotokea.

Tume mpya imepewa jukumu la kwenda hatua zaidi kwa kuchunguza wahusika wa ghasia hizo, namna walivyoshiriki na kiwango cha nguvu kilichotumika katika kudhibiti vurugu hizo.

Jaji Lila amesema Tume pia itachunguza madhara yaliyotokana na ghasia hizo, yakiwemo vifo, majeruhi na watu waliopotea.

Amesema Tume iliyokuwa chini ya Jaji Chande ilibainisha vifo vya watu 518, huku ikieleza kuwa huenda idadi hiyo ilikuwa kubwa zaidi kwa sababu si waathirika wote waliweza kufikiwa au kutambuliwa.

Katika utekelezaji wa majukumu yake, Tume ya Jaji Lila imepewa hadidu tano za rejea.

Hadidu ya kwanza ni kuchunguza na kubainisha wahusika wa ghasia na namna walivyoshiriki katika kupanga, kufadhili, kuratibu au kutekeleza matukio hayo.

Hadidu ya pili ni kuchunguza matukio mahsusi yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi, ikiwemo madai ya vifo visivyo vya kawaida vya watoto na watu wa makundi maalum.

Hadidu ya tatu ni kuchunguza taarifa za watu waliopotea katika maeneo yaliyokumbwa na ghasia na uvunjifu wa amani.

Hadidu ya nne ni kuchunguza madai ya matumizi ya nguvu kupita kiasi na kubaini iwapo taratibu na miongozo ya matumizi ya nguvu ilizingatiwa.

Hadidu ya tano inalipa Tume nafasi ya kuchunguza suala lolote litakaloonekana kuwa muhimu na linalohusiana na majukumu yake.

Jaji Lila amesema Tume imeundwa na Rais Samia Suluhu Hassan na kuzinduliwa rasmi Agosti 7, 2026.

Tume hiyo inaongozwa na Jaji Mstaafu Shaban Ally Lila na inajumuisha majaji wastaafu wa Mahakama Kuu, akiwemo Jaji Gad Mjemmas, Jaji Awadh Bawazir na Jaji Aishieli Sumari, pamoja na wajumbe kutoka nje ya Tanzania, akiwemo Naibu Jaji Mkuu wa Namibia na Jaji Cheborion Barishaki kutoka Uganda.

Leave a Comment