×

Uingereza Yakanusha Taarifa ya Shambulio la Mtandaoni la Iran

Serikali ya Uingereza imekanusha taarifa iliyochapishwa na gazeti la Telegraph kuhusu shambulio la mtandaoni linalodaiwa kufanywa na Iran dhidi ya kituo cha kuzalisha umeme nchini humo, ikisema tukio hilo liliathiri jenereta ndogo ya nishati na si kiwanda cha umeme.

Gazeti la Telegraph liliripoti kwamba Iran ilikuwa imefanikiwa kuingia katika mfumo wa kituo cha umeme nchini Uingereza kwa siku nne katika shambulio la mtandaoni lililoelezwa kuwa “lisilo na kifani.”

Hata hivyo, msemaji wa Serikali ya Uingereza amesema mfumo wa nishati wa nchi hiyo unaendelea kuwa imara na kwamba hakukuwa na tishio lolote dhidi ya mfumo mkuu wa nishati.

Vyanzo vya Serikali ya Uingereza pia vimeeleza kuwa taarifa ya Telegraph ilitiwa chumvi, huku vikisisitiza kwamba tukio hilo halikuhusisha mitambo mikubwa ya kuzalisha umeme.

Uingereza imesema baada ya tukio hilo, Idara ya Usalama wa Nishati iliwafahamisha viongozi wa juu katika kampuni za nishati kuhusu tukio hilo na kuwapatia mapendekezo pamoja na mwongozo kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa.

Kituo cha Kitaifa cha Usalama wa Mtandaoni cha Uingereza pia kinahusika katika kushughulikia matukio makubwa ya mtandao, pamoja na kuratibu majibu ya Serikali na mashirika yaliyoathiriwa.

Hatua hizo zinaendelea kuchukuliwa wakati Uingereza ikiimarisha ulinzi wa miundombinu yake muhimu dhidi ya vitisho vya mtandaoni.

Leave a Comment