Ukiambiwa kuna kanisa ambalo ujenzi wake umechukua zaidi ya miaka 140 na bado haujakamilika, huenda ukashangaa. Lakini hali hiyo ipo katika jiji la Barcelona nchini Hispania, ambako kuna kanisa maarufu la Sagrada Família.
Ujenzi wa kanisa hilo ulianza mwaka 1882, kabla ya mbunifu Antoni Gaudí kuchukua jukumu la kuendeleza usanifu wake. Gaudí alilitumia sehemu kubwa ya maisha yake katika kulibuni na kulisimamia, lakini alifariki mwaka 1926 kabla ya kukamilika.
Baada ya kifo chake, ujenzi uliendelea kwa kutegemea michango na misaada ya watu binafsi. Hata hivyo, safari ya ujenzi haikuwa rahisi.
Mwaka 1936, wakati wa Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Hispania, sehemu ya nyaraka, michoro na vielelezo vya Gaudí ziliharibiwa, jambo lililosababisha changamoto kubwa kwa waendelezaji wa mradi huo katika kujaribu kufuatilia maono yake ya awali.
Kutokana na ukubwa na ugumu wa usanifu wa jengo hilo, pamoja na mabadiliko yaliyotokea kwa miaka mingi, ujenzi umeendelea kwa hatua tofauti hadi sasa.

Sagrada Família liliwekwa wakfu mwaka 2010 na kutangazwa kuwa basilika ndogo, huku likifunguliwa rasmi kwa umma.
Kinacholifanya kanisa hilo kuwa la kipekee ni kwamba hata baada ya kutumika kwa ibada na kutembelewa na watalii kutoka sehemu mbalimbali duniani, baadhi ya sehemu zake bado zinaendelea kujengwa.
Kwa hiyo, zaidi ya miaka 140 tangu kuwekwa jiwe la msingi, Sagrada Família bado linaendelea kuwa moja ya miradi mikubwa ya usanifu na ujenzi duniani, likibeba historia ndefu ya maono ya Antoni Gaudí na vizazi vilivyokuja baada yake.
