
Msanii wa kimataifa kutoka Marekani, Cardi B, amepewa nafasi ya kipekee kwenye jalada la toleo la Septemba 2026 la Vogue Arabia, katika picha iliyozua gumzo kutokana na mtindo wake wa kipekee wenye mguso wa utamaduni wa Kiarabu.
Jalada hilo, lililotolewa Agosti 27, 2026, linamuonyesha Cardi B akiwa amevalia vazi la kifahari lenye mchanganyiko wa rangi nyeusi na kijani, huku akiwa ameshikilia tufaha.
Kinachovutia zaidi ni ujumbe ulioandikwa kwenye jalada hilo, “Assalamu Alaikum, Cardi B”, ambao umeongeza mvuto wa picha hiyo na kuonyesha namna msanii huyo anavyoendelea kuhusishwa na utamaduni wa eneo la Arabia.
Katika toleo hilo, Vogue Arabia imemzungumzia Cardi B kwa upana, ikigusa safari yake ya muziki, mitindo, umaarufu pamoja na maisha yake nje ya jukwaa akiwa mama.

Jarida hilo limemuelezea kama msanii mwenye uwezo mkubwa wa kubadilika kimtindo bila kupoteza utambulisho wake.
Cardi B naye ameonyesha furaha yake kupitia mitandao ya kijamii, ambapo amewashukuru Vogue Arabia pamoja na mpiga picha na mkurugenzi wa ubunifu Szilveszter Makó kwa kazi hiyo.
Mwonekano wake umeendelea kuzungumziwa na mashabiki kwenye mitandao ya kijamii, wengi wakimpongeza kwa kuonekana tofauti na vile walivyozoea kumuona kwenye matukio mbalimbali.
Cardi B si mgeni katika eneo la Mashariki ya Kati. Amewahi kutembelea Saudi Arabia na kutumbuiza katika tamasha la MDLBEAST Soundstorm jijini Riyadh.
Safari hiyo pia ilimpa nafasi ya kueleza hisia zake kuhusu watu na utamaduni wa Saudi Arabia, huku akionyesha kuvutiwa na baadhi ya vipengele vya utamaduni huo.
Kwa jalada hili la Vogue Arabia, Cardi B anaendelea kuonyesha kuwa ushawishi wake hauishii kwenye muziki pekee, bali pia unaendelea kukua katika mitindo, utamaduni na burudani ya kimataifa.
Stori na Nasra Kassim | GPL – TUDACO