
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za rambirambi kwa wananchi na Serikali ya Norway kufuatia kifo cha aliyekuwa Mfalme wa taifa hilo, Harald V, aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 89.
Kupitia ujumbe wake rasmi, Rais Samia ameeleza kusikitishwa kwake na taarifa hizo huku akiihakikishia familia ya kifalme na wananchi wa Norway kuwa Tanzania ipo pamoja nao katika kipindi hiki cha simanzi kuu.
“Nimesikitishwa sana na taarifa za kifo cha Mheshimiwa Mfalme Harald V wa Norway. Kwa niaba ya Serikali na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninatuma rambirambi zetu za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Mfalme Haakon VIII, Familia ya Kifalme, na wananchi wa Ufalme wa Norway,” alisema Rais Samia.
Mfalme Harald V, aliyekuwa mfalme wa umri mkubwa zaidi barani Ulaya, amefariki dunia katika Hospitali ya Taifa ya Oslo (Rikshospitalet). Kufuatia msiba huo, Mwana wa Mfalme, Prince Haakon, anatarajiwa kuchukua mikoba ya uongozi kama Mfalme mpya wa taifa hilo.
Ikumbukwe kuwa Tanzania na Norway zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu wa kidiplomasia na kiuchumi, na ujumbe wa Rais Samia unadhihirisha mshikamano thabiti kati ya mataifa haya mawili.
Na Hasina Thabit