×

Askari Polisi Afariki Akiwa Mahabusu Kituo Cha Polisi Tanga

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Almachius Mchunguzi.

Tanga — Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limethibitisha kifo cha askari wake, H.1796 Koplo Mwita, aliyekuwa akishikiliwa kwa ajili ya uchunguzi katika Kituo cha Polisi Wilaya ya Tanga.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, tarehe 27 Agosti 2026 majira ya saa 1:03 usiku, Koplo Mwita alifariki dunia akiwa ndani ya chumba cha mahabusu katika kituo hicho.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa kabla ya kifo chake, marehemu pamoja na afisa mmoja na askari watano wa Jeshi la Polisi wa vyeo mbalimbali walikuwa wakishikiliwa kwa tuhuma za kijinai.

Jeshi la Polisi limesema baada ya kifo hicho, uchunguzi wa kisayansi uliofanywa na ndugu wa marehemu kushuhudia umebaini kuwa chanzo cha kifo kilikuwa kukosa hewa kutokana na kujinyonga.

Aidha, mwili wa marehemu umebakizwa na ndugu zake kwa ajili ya taratibu za mazishi, huku Jeshi la Polisi likisema linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

Katika taarifa hiyo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limewataka wananchi, waandishi wa habari na watumiaji wa mitandao ya kijamii kuepuka kuanzisha au kusambaza taarifa zisizothibitishwa, pamoja na kutoa hitimisho lisilotokana na matokeo rasmi ya uchunguzi.

Jeshi hilo limeeleza kuwa kufanya hivyo ni upotoshaji ambao ni kinyume cha sheria.

Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limesisitiza kuwa linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na litahakikisha taratibu zote za kiuchunguzi zinafuatwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.

Imetolewa na Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Tanga, Agosti 31, 2026.

Leave a Comment