×

Mwanamke Akamatwa kwa Tuhuma za Kumuua Mumewe – Video

Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limemkamata Jovita Bateguye Budyo, mwenye umri wa miaka 30, kwa tuhuma za kumuua mumewe, Abeli Charles, mwenye umri wa miaka 44, katika eneo la Mafisa, Morogoro Mjini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, tukio hilo lilitokea usiku wa Agosti 31, 2026, katika Mtaa wa Mafisa kwa Mambi, Kata ya Mafisa, Wilaya ya Morogoro Mjini, ambako mtuhumiwa na marehemu walikuwa wakiishi pamoja.

Taarifa inaeleza kuwa wawili hao walikuwa wakijiandaa kwenda kulala kabla ya kutokea kwa mgogoro wa kifamilia unaodaiwa kuhusishwa na suala la kunyimwa unyumba.

Inadaiwa kuwa mgogoro huo ulisababisha ugomvi, ambapo mtuhumiwa anadaiwa kumkata marehemu kwa kitu chenye ncha kali katika maeneo ya shingoni na kichwani.

Kutokana na majeraha hayo, Abeli Charles alifariki dunia.

Baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi lilimkamata Jovita na linaendelea na uchunguzi pamoja na hatua nyingine za kisheria kuhusu tukio hilo.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limewataka wananchi kutumia njia salama katika kutatua migogoro ya kifamilia na mahusiano, badala ya kutumia nguvu au vitendo vya ukatili.

Aidha, wananchi wameshauriwa kuwashirikisha watu wanaowaamini, wazee wenye busara au vyombo vya sheria wanapokabiliwa na migogoro ili kuzuia matukio yanayoweza kusababisha madhara au kupoteza maisha.

Stori na Lailath Burhan | GPL

Leave a Comment