×

Ndejembi Awasalimu Wananchi Moshi, Atoa Ahadi Kwa Rais Samia

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, amewasalimu wananchi wa Mbuyuni wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro, waliokusanyika kumpokea alipokuwa katika ziara binafsi mkoani humo leo, Septemba 1, 2026.

Akizungumza na wananchi hao, Makamu wa Rais amewasihi kuendelea kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na yeye binafsi, ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Mhe. Ndejembi amesema kupitia nguvu ya maombi ataweza kumsaidia Rais Samia kwa hekima na utii katika kutekeleza majukumu ya kuwatumikia wananchi.

Aidha, amesema ataendelea kutekeleza wajibu wake kwa uadilifu, umakini na kujituma, huku akisisitiza utayari wake wa kushirikiana na viongozi pamoja na wananchi katika kutekeleza majukumu ya kitaifa.

Akizungumza kwa msisitizo, Makamu wa Rais amesema:

“Hatawazingua Wana wala hatamzingua Mama,”

kauli ambayo alisema aliitoa pia mkoani Dodoma kwa wananchi wa Chamwino mara baada ya kuapishwa.

Kabla ya kuelekea Mbuyuni, Makamu wa Rais aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), ambako alipokelewa na viongozi mbalimbali wa Serikali, viongozi wa dini pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Kilimanjaro.

 

Leave a Comment